Hatua mpya ya Wamagharibi ya kuchochea moto wa vita vya Ukraine
(last modified Mon, 18 Nov 2024 11:13:50 GMT )
Nov 18, 2024 11:13 UTC
  • Hatua mpya ya Wamagharibi ya kuchochea moto wa vita vya Ukraine

Rais wa Marekani, Joe Biden ameripotiwa kuidhinisha Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya Kimarekani kulenga shabaha ndani ya mipaka ya Russia ya kabla ya 2014. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya jana Jumapili iliyotolewa na gazeti la New York Times likiwanukuu maafisa wa Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina yao.

Maafisa watatu ambao hawakutaka kutajwa majina yao wamefichua kuwa, Biden amebadilisha siasa za Marekani kuhusu vita baina ya Russia na Ukraine na ameondoa marufuku ya serikali ya Kyev ya kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani kupiga maeneo ya ndani kabisa ya Russia.

Hatua ya serikali ya Biden ambaye baada ya takriban miezi miwili hatokuwa tena rais wa Marekani imechukuliwa baada ya maombi ya miezi mingi ya rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy ya kuitaka Marekani imruhusu kutumia makombora ya nchi hiyo kupiga maeneo ya ndani ya nchi ya Russia. 

Kwa upande wake gazeti la Le Figaro la nchini Ufaransa limeripoti kuwa, baada ya White House kuiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani kupiga maeneo ya ndani ya Russia, nchi nyingine mbili za Magharibi yaani Ufaransa na Uiingereza nazo zimeiruhusu Ukraine kutumia silaha zao kushambulia maeneo ya ndani kabisa ya ardhi ya Russia.

Marais wa Marekani na Ukraine

 

Mara kwa mara, rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amekuwa akiwaomba viongozi wa nchi za Marekani wamruhusu kutumia silaha wanazompa kushambulia viwanja vya ndege, vituo vya kuvurumishia makombora vya Russia pamoja na maghala ya silaha na vituo vya mafua vya Russia. Andrii Ivanovych Sybiha, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine naye amesema kuwa, idhini iliyotolewa kwa Ukraine hivi sasa ni muhimu sana kwani kuanzia sasa hakutakuwa na kizuizi chochote cha nchi yake kutumia silaha za nchi za Magharibii kupiga sehemu yoyote inayotaka ndani ya ardhi ya Russia. 

Hatua hiyo ya madola ya Magharibi imechukuliwa baada ya mivutano ya muda mrefu. Hatua hiyo inaonesha kuweko mabadiliko ya kimsingi katika misimamo ya nchi tatu zenye ushawishi mkubwa ndani ya Jeshi la Nchi za Magharibi NATO yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa. Inaonesha wazi kuwa lengo la nchi hizo ni kuchochea vurugu na vita vya Ukraine. Nchi hizo zimeipa idhini Ukraine kutumia inavyotaka silaha inazopewa na nchi za Magharibi kupiga sehemu yoyote inayotaka ndani ya ardhi ya Russia.

Mji mkuu wa Ukraine ulivyochakazwa vibaya na vita

 

Hatua hiyo ya nchi za Magharibi imekuja baada ya maonyo makali ya mfululizo yanayotolewa na Moscow kuhusu hatua ya kutumiwa silaha za Magharibi kushambulia ardhi ya Russia. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, hatua hiyo inaonesha wazi kwamba Joe Biden amekusudia kumuweka rais ajaye wa Marekani, Donald Trump katika mazingira magumu wakati atakapoingia madarakani nchini humo tarehe 20 Januari 2025. Wachambuzi hao wanasema kuwa, inaonekana wazi kwamba lengo la serikali ya Biden ni kuhakikisha Trump hapati nafasi ya kulegeza kamba kwa namna yoyote ile mbele ya Russia wakati wa utawala wake huko Marekani.

Kabla ya hapo Rais Vladimir Putin wa Russia alisema kuwa, kuruhusiwa Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu inayopewa na madola ya Magharibi kushambulia ardhi za Russia, kuna maana ya kushiriki moja kwa moja nchi za NATO katika vita hivyo na kwamba hatari za jambo hilo hazitabiriki hata kidogo. Matamshi hayo ya Rais wa Russia yanahesabiwa kuwa ni onyo la moja kwa moja kwa madola ya Magharibi hasa Marekani, Uingereza na Ufaransa kwamba Moscow nayo itazihesabu ardhi za nchi hizo kuwa ni uwanja wa vita kama ilivyo Ukraine.