Maandamano ya watetezi wa Palestina yaendelea ulimwenguni
Wafuasi wa wananchi na wanachuo wa Palestina katika baadhi ya nchi wametoa wito wa kukomeshwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza na Lebanon kwa mikusanyiko na maandamano.
Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina na kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel yameendelea kushuhudiwa katika mataifa mbalimbali hususan barani Ulaya.
Mataifa ya Canada, Uholanzi, Uingereza, Italia, Ubelgiji na Ujerumani yameendelea kushuhudia maandamano makubwa ya waungaji mkono wa Palestina.
Waandamanani hao wamekuwa wakipiga nara dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wao na kutoa mwito wa kukomeshwa jinai na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Aidha maandamano kama hayo yameshuhudiwa nchini Ireland. Waandamanaji nchini humo wamekosoa vikali sera za serikali ya Marekani na madola ya Magharibi kwa ujumla ya kuusaidia utawala vamizi wa Israel unaofanya mauaji kila uchao dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Wakati huohuo, Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa: tangu vilipoanza vita vya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa imefikia 44,056 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia 104,268.