Mrusi aliyehukumiwa kwa kuchoma nakala ya Quran, afungwa miaka 14 jela kwa kosa la uhaini
(last modified Tue, 26 Nov 2024 13:53:51 GMT )
Nov 26, 2024 13:53 UTC
  • Mrusi aliyehukumiwa kwa kuchoma nakala ya Quran, afungwa miaka 14 jela  kwa kosa la uhaini

Mwanaume mmoja raia wa Russia aliyepatikana na hatia ya kuchoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Waislamu, Qur'ani, mapema mwaka huu, amehukumiwa kifungo cha ziada cha miaka 14 jela kwa kosa la uhaini.

Shirika la habari la serikali ya Russia, Tass limeandika kuwa Nikita Zhuravel amehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela baada ya kesi yake kusikiliza katika mji wa Volgograd.

Mahakama ya Mkoa ya Volgograd ilimruhusu kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, na wakili wa Zhuravel akaelezea nia ya mteja wake kufanya hivyo.

Mwezi uliopita, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Russia ilisema katika taarifa kwamba ofisi yake ya mkoa wa Volgograd iliidhinisha mashtaka katika kesi ya Zhuravel.

Kulingana na wale wanaochunguza kesi hiyo, Zhuravel alikuwa jasusi wa Shirika la Kijasusi la Ukraine ambaye alikuwa akitoa taarifa kuhusu jeshi la Russia.

Mapema mwezi Februari, Zhuravel alipokea kifungo cha miaka mitatu na nusu baada ya kuzuiliwa Mei 2023 kwa kuchoma nakala ya Qur'ani Tukufu mbele ya msikiti wa Volgograd.