Magaidi waua makumi ya askari wa Mali Timbuktu, Boulkessi
Kundi la kigaidi lenye mafungamano na mtandao wa Al Qaeda katika eneo la Sahel, Magharibi mwa Afrika limedai kufanya mashambulizi kadhaa nchini Mali na kuua makumi ya wanajeshi.
Katika shambulio la jana Jumatatu, genge hilo la kigaidi linaloojita Jama'a Nusrat ul-Islam wa al-Muslimin (JNIM), lilisema limeshambulia uwanja wa ndege wa kijeshi na mamluki wa Russia katika mji wa Boulkessi eneo la kati la Douentza na kuua askari kadhaa.
Habari zaidi zinasema kuwa, wakaazi wa eneo hilo walilazimika kujificha kutokana na kupamba moto makabiliano ya risasi baina ya wanajeshi wa Mali na wanamgambo hao.
Wakati huo huo, shirika la habari la Reuters limenukuu vyanzo viwili vikisema kuwa, magaidi hao waliua zaidi ya wanajeshi 30 katika shambulio la Jumapili katika mji wa kaskazini wa Timbuktu.
Hata hivyo, Kikosi cha Wanajeshi wa Mali (FAMa) jana Jumatatu kilisema kilitibua "jaribio la kujipenyeza la wapiganaji wa kigaidi" katika kambi ya kijeshi ya Timbuktu kaskazini mwa Mali, ambapo magaidi 13 "wameangamizwa," na silaha, magari na zana mbalimbali kutwaliwa.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jeshi la Mali lilitangaza kuwa limeua magaidi 21 wakati wa operesheni zake kwenye eneo la Sebabougou la magharibi mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Mwezi Februari mwaka huu, Jeshi la Mali lilitangaza kuwa raia 25 wameuawa na wengine 13 kujeruhiwa; aghalabu yao wakiwa ni wachimba madini vijana wa nchi za kigeni. Hali kadhalika "miili ya magaidi 19 ilipatikana katika eneo la tukio," ilieleza taarifa ya jeshi la Mali.