Mbunge Uhispania ashiriki mgomo wa kula kuunga mkono Palestina
Mbunge mmoja nchini Uhispania, Jorge Pueyo, ametangaza kushiriki katika mgomo wa kula chakula ikiwa ni njia ya kuunga mkono wananchi wa Palestina waliozingirwa na kunyimwa chakula huko Gaza.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 29 amesema alijiunga na mgomo ulioanzishwa na Jumuiya ya ya Palestina ya Aragon na Taasisi ya Jerusalem (Quds) mnamo Novemba 19 katika eneo bunge lake- ambalo ni eneo lenye mamlaka ya ndani la Aragon.
Amesema katika mkutano na waandishi wa habari bungeni kwamba alianza mgomo wake wa kula Jumanne kuonyesha mshikamano na Palestina na atauendeleza hadi Ijumaa.
Akifafanua kuhusu uamuzi wake amesema: "Kuna nyakati katika maisha na siasa ambapo maneno hayatoshi, na kuweka mfano inakuwa muhimu."
Mbunge huyo mchanga pia ametoa wito kwa Uhispania kukata uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara na Israel, kuweka vikwazo kamili vya silaha dhidi ya utawala wa Tel Aviv, na kuhimiza kusambaza taarifa kuhusu kadhia ya Palestina. Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez alitangaza msimamo wa nchi yake wa kulitambua rasmi taifa la Palestina mwezi Mei.
Sánchez alisema wakati huo kwamba nchi yake " itajiunga na zaidi ya nchi 140 ambazo tayari zinaitambua Palestina kama nchi."
Nchi nyingi za Ulaya, kama vile Ireland na Norway, zilifuata kampeni ya kutaka kumaliza vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza.