Putin amwambia Merkel: Nisamehe, sikujua kuwa unaogopa mbwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i119532-putin_amwambia_merkel_nisamehe_sikujua_kuwa_unaogopa_mbwa
Rais wa Russia, Vladimir Putin, amemuomba radhi Kansela wa zamani wa Ujerumani, Angela Merkel, akisisitiza kwamba hakumtisha kwa makusudi alipomuingiza mbwa wake katika mkutano waliofanya mwaka 2007, baada ya Merkel kuandika tukio hilo katika kitabu cha kumbukumbu zake kilichochapishwa hivi majuzi.
(last modified 2024-11-30T07:51:50+00:00 )
Nov 30, 2024 07:51 UTC
  • Putin na Merkel
    Putin na Merkel

Rais wa Russia, Vladimir Putin, amemuomba radhi Kansela wa zamani wa Ujerumani, Angela Merkel, akisisitiza kwamba hakumtisha kwa makusudi alipomuingiza mbwa wake katika mkutano waliofanya mwaka 2007, baada ya Merkel kuandika tukio hilo katika kitabu cha kumbukumbu zake kilichochapishwa hivi majuzi.

Putin aliwaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake huko Astana Allhamisi iliyopita kwamba: "Sikujua kwamba anaogopa mbwa", na kuongeza kuwa: "Nazungumza tena naye kupitia vyombo vya habari nikisema, Angela, naomba unisamehe. Sikutaka kukusababishia maumivu yoyote. Kinyume chake, nilitaka kutengeneza mazingira yanayofaa kwa ajili ya mazungumzo yetu." 

Wakati wa mkutano wao mwaka 2007 katika mji wa Sochi kusini mwa Russia, mbwa mweusi aina ya labrador retriever ambaye Putin alimuita "Koni" aliingia kwenye chumba cha mkutano na kumkaribia Merkel, ambaye alikuwa akitabasamu lakini kwa wahka na wasiwasi.

Kansela huyo wa zamani wa Ujerumani ameandika katika kumbukumbu zake kwamba: "Ilikuwa wazi katika sura ya Putin kwamba alikuwa akifurahia yaliyokuwa yakijiri."