Vitisho vya Trump dhidi ya mataifa wanachama wa BRICS
Dec 02, 2024 23:19 UTC
Donald Trump, rais mteule wa Marekani, amezitishia nchi wanachama wa kundi la BRICS kwamba ikiwa zitajaribu kuanzisha sarafu nyingine itakayokuwa mbadala wa dola ya Marekani, ataziwekea bidhaa zao ushuru wa kibiashara wa 100%.
Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa TruthSocial kwamba, wanachama wa BRICS wanapaswa waahidi kuwa hawatoanzisha sarafu mpya kwa ajili ya BRICS na hawataunga mkono sarafu nyingine ya kuchukua nafasi ya dola ya Marekani; vinginevyo, watakabiliwa na ushuru mkubwa na itawapasa waliage soko la Marekani.
BRICS ni shirika la kimataifa, ambalo wanachama wake ni Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini, Misri, Ethiopia, Muungano wa Falme za Kiarabu na Iran. Shirika hilo ambalo hapo awali liliundwa kwa ajili ya kuangazia fursa za uwekezaji, lilibadilika na kuwa kambi ya kijiopolitiki; na tangu mwaka 2009 nchi zake wanachama zimekuwa zikifanya mikutano rasmi kila mwaka na kuratibu kwa pamoja sera za kimataifa za baina ya pande kadhaa.
Trump ametoa vitisho dhidi ya wanachama wa BRICS wakati kimsingi, moja ya malengo makuu ya kuundwa kundi hilo ni kukabiliana na ukiritimba wa sarafu ya dola ya Marekani na kutumiwa kwake kama silaha ya kiuchumi ya kutoa mashinikizo na vitisho dhidi ya nchi nyingine.
Ukweli ni kuwa, tangu wanachama wa awali wa BRICS walipounda kundi hilo mwaka 2009, walitaka kuhitimisha 'ubabe' wa sarafu ya dola na nguvu za kiuchumi za Magharibi katika miamala ya kibiashara. Suala la kutumia sarafu nyingine badala ya dola, siku zote limekuwa ndilo dukuduku la nchi wanachama wa BRICS, na dukuduku hilo limeongezeka zaidi katika miaka ya karibuni, ambapo nchi wanachama zimefanya jitihada za kuiondoa dola kwenye miamala yao ya kibiashara. Nchi hizo zimo mbioni kuhakikisha kuwa, sambamba na kupunguza utegemezi wa kimataifa kwa sarafu ya dola ya Marekani pamoja na yuro ya Ulaya, zinapiga hatua zitakazozaa matunda kwa manufaa ya chumi zao.
Katika mkutano wa kilele wa BRICS uliofanyika hivi karibuni huko Kazan, Russia, Moscow ilitoa taarifa ya kuhimiza kuimarishwa "mitandao ya baina ya mabenki ndani ya BRICS na kurahisisha ufanyaji miamala ya malipo ndani ya nchi wanachama kulingana na ubunifu wa ufanyaji miamala nje ya mipaka ya BRICS". Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov alitangaza kuwa, nchi za BRICS zinatayarisha mifumo salama ya miamala ya malipo kuchukua nafasi ya dola.
Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa ikiitumia dola kama silaha na chombo cha kuzilazimishia nchi nyingine kufuata sera za Washington. Hatua iliyochukuliwa na Marekani katika miaka ya karibuni ya kuziwekea vikwazo vikubwa vya kiuchumi nchi kama Iran, Russia na Venezuela ni mfano mmojawapo wa kuitumia sarafu ya dola kama wenzo wa kimaslahi.
Akizungumzia kudhoofika kwa nguvu na ukiritimba wa sarafu ya dola duniani, mwanasiasa na mbunge wa Ujerumani Sevim Dağdelen amesema, kadiri dola inavyozidi kuondolewa kwenye mzunguko wa shughuli za fedha kama sarafu kuu duniani, ndivyo kasi ya kuelekea kwenye ulimwengu wa pande kadhaa inavyoongezeka licha ya upinzani wa nchi wanachama wa NATO.
Ndani ya Marekani kwenyewe, wataalamu wengi wameshatoa indhari ya kufikia kikomo ukritimba wa sarafu ya dola.
Mwanauchumi mtajika wa Marekani na profesa katika Chuo Kikuu cha Columbia, Jeffrey Sachs, amesema, ukiritimba wa Marekani umemalizika kwa maana yake pana katika nyuga za kisiasa na kiuchumi; na akafafanua kuwa, -kutokana na ukuaji wa nchi nyingine, maendeleo ya kidijitali na kutumia kimaslahi Marekani nafasi ya sarafu yake ya taifa ikiwa ndio sarafu ya kimataifa, sambamba na kuitumia vibaya kama silaha katika kuziwekea vikwazo Russia, Iran, Venezuela na nchi nyinginezo-, wigo wa matumizi ya dola unatarajiwa kupungua kwa kiasi kikubwa. Akizungumzia kuachana Russia na utumiaji wa sarafu ya dola katika miamala ya kibiashara na China na Brazil, mwanauchumi huyo amesema: "Hii inaharakisha mchakato wa kujivua na utegemezi wa dola".
Kufifia kwa nguvu ya dola ni suala ambalo viongozi wa Marekani, akiwemo hata Trump mwenyewe wanalifahamu vyema. Kabla ya uchaguzi wa rais, Trump aliwahi kutahadharisha kuhusu kudhoofika kwa ukiritima wa dola duniani na akasema: kuporomoka kwa hadhi ya dola kama akiba ya dunia ya fedha za kigeni ni kushindwa kukubwa zaidi kuliko kushindwa katika vita vyovyote vile.
Hata hivi sasa pia, rais huyo mteule wa Marekani amejaribu kutoa vitisho dhidi ya nchi wanachama wa BRICS ili kusimamisha mchakato wa kutafuta sarafu itakayochukua nafasi ya dola, jambo linalodhihirisha hofu na wasiwasi alionao Trump juu ya suala hilo.
Lakini pamoja na vitisho hivyo, inavyoonekana sera ya kuachana na dola si kitu kitachoweza kusimamishwa; bali ni kinyume chake, kwamba vitisho hivyo vitazidi kuzifanya nchi hizo ziwe na azma thabiti zaidi ya kuendeleza mchakato wa kuiweka kando sarafu hiyo ya Marekani.../