Mashirika ya silaha ya Marekani yazidi kujitajirisha kwenye dimbwi la damu
Takwimu za hivi karibuni kabisa zilizotolewa na taasisi ya amani ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI) zinaonesha kuwa, mashirika yanayozalisha silaha duniani ambayo asilimia kubwa ni ya Marekani, yamepata faida kubwa kupindukia kwa kuuza silaha zilizoishia kumwaga damu za watu kwenye kona mbalimbali za dunia hasa barani Asia.
Shirika la habari la Tasnim limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, takwimu za hivi karibuni kabisa zilizotolewa na taasisi ya amani ya SIPRI zinaonesha kuwa, mwaka 2023 kulikuwa na uzalishaji karibu 100 wa idadi kubwa kupindukia ya silaha duniani ambazo zilikuwa na thamani ya dola bilioni 632 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.2 ikilinganishwa na uzalishaji na uuzaji wa silaha katika mwaka wa kabla yake wa 2022.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa taasisi hiyo, karibu nusu ya mauzo ya silaha duniani yanafanywa na mashirika ya kutengeneza silaha ya Marekani. Mwaka 2023 mashirika hayo yaliongeza asilimia 2.5 ya uzalishaji silaha ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake na kutia kibindoni dola bilioni 317 kwa uuzaji silaha ndani na nje ya Marekani, silaha ambazo zinatumika kufanya mauaji ya umati na maangamizi ya kizazi kama huko Ghaza na Lebanon.
Hayo yameripotiwa katika hali ambayo kiwango cha misaada ya kifedha kilichotengwa na Congress ya Marekani mwaka jana kwa ajili ya Ukraine baada ya kuanza vita vyake na Russia, kilipindukia dola bilioni 182.
Gazeti la Washington Post limeandika kuwa, ukiachilia mbali fedha nyingi zinazotumiwa na Marekani kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel, Washington imeongeza mno fedha inazoumiminia utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba 2023 yalipoanza mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya wakazi wa Ghaza huko Palestina.