Upinzani nchini Korea Kusini wataka Rais auzuliwe, umeapa kumfungulia mashtaka
https://parstoday.ir/sw/news/world-i119702-upinzani_nchini_korea_kusini_wataka_rais_auzuliwe_umeapa_kumfungulia_mashtaka
Chama kikuu cha upinzani nchini Korea Kusini kimetangaza - leo, Jumatano - kwamba kimewasilisha ombi la kumuondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol, baada ya kutangaza nia yake ya kumfungulia mashitaka pamoja na wasaidizi wake wakuu wa masuala ya usalama kwa tuhuma za "uasi," kufuatia hatua yake ya kutangaza sheria za kijeshi nchini, hatua ambayo ilizuiliwa haraka na Bunge.
(last modified 2024-12-04T09:21:04+00:00 )
Dec 04, 2024 09:21 UTC
  • Upinzani nchini Korea Kusini wataka Rais auzuliwe, umeapa kumfungulia mashtaka

Chama kikuu cha upinzani nchini Korea Kusini kimetangaza - leo, Jumatano - kwamba kimewasilisha ombi la kumuondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol, baada ya kutangaza nia yake ya kumfungulia mashitaka pamoja na wasaidizi wake wakuu wa masuala ya usalama kwa tuhuma za "uasi," kufuatia hatua yake ya kutangaza sheria za kijeshi nchini, hatua ambayo ilizuiliwa haraka na Bunge.

Wawakilishi wa vyama sita vya upinzani vinavyoongozwa na Chama cha Demokrasia, chama maarufu zaidi cha upinzani, wamesema: "Tumewasilisha ombi la kuuzuliwa Rais" wakieleza kwamba watachunguza baadaye tarehe ya kuwasilishwa ombi hilo bungeni kwa ajili ya kupiga kura, ambayo inaweza kufanyika Ijumaa ijayo.

Chama cha Demokrasia pia kimetangaza kwamba kitawasilisha kesi mahakamani dhidi ya Rais wa Jamhuri, Mawaziri wa Ulinzi na Mambo ya Ndani, na viongozi muhimu katika jeshi na polisi waliohusika katika kutangaza hali ya sheria ya kijeshi, kwa tuhuma za uasi.

Kimeongeza kuwa tangazo la Yoon la sheria ya kijeshi "ni ukiukaji wa wazi wa Katiba."

Kwa upande wake, kiongozi wa chama tawala nchini Korea Kusini ameutaja uamuzi wa Rais wa kutangaza sheria ya kijeshi nchini humo kuwa "majanga," akitaka kuwajibishwa wale wote waliohusika na jaribio hilo ambalo amelitaja kuwa limefeli.

Yoon Suk Yeol

Kufuatia hatua ya Rais Yoon Suk Yeol ya kutangaza sheria ya kijeshi, ambayo ilifutwa baada ya saa 6, maafisa wakuu katika ofisi ya rais mjini Seoul, akiwemo mkuu wa timu ya rais, waliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa pamoja, mapema  leo.

Rais Yoon alitangaza sheria ya kijeshi kwa kisingizio cha "kuitetea Korea Kusini dhidi ya Korea Kaskazini na eti kulinda "utawala huru wa kikatiba."

Kambi ya upinzani nchini Korea Kusini imemtuhumu Rais Yoon Suk Yeol kuwa ametangaza hali ya dharura ya sheria ya kijeshi ili kumlinda mke wake, Kim Keon-hee, aliye chini ya uchunguzi wa vyombo vya dola.

Kim anachunguzwa kwa madai ya kupokea begi ya Christian Dior yenye thamani ya $2,200 kama zawadi, jambo ambalo linaweza kutambuliwa kuwa ni ukiukaji wa sheria ya kupambana na ufisadi nchini Korea Kusini.