WHO yalaani mauaji yaliyotekelezwa na Israel hospitalini Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i119818-who_yalaani_mauaji_yaliyotekelezwa_na_israel_hospitalini_gaza
Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa WHO limeonya kwamba mashambulizi ya Israel yanayoendelea Kaskazini mwa Gaza yanaendelea kuzuia upatikanaji wa huduma muhimu za afya zinazohitajika sana.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Dec 07, 2024 03:21 UTC
  • WHO yalaani mauaji yaliyotekelezwa na Israel hospitalini Gaza

Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa WHO limeonya kwamba mashambulizi ya Israel yanayoendelea Kaskazini mwa Gaza yanaendelea kuzuia upatikanaji wa huduma muhimu za afya zinazohitajika sana.

Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa mjini Geneva Uswisi Dkt. Richard Peeperkorn ambaye ni mwakilishi wa WHO katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Palestina  amesema “Ufikiaji wa hospitali za Kamal Adwan, Al Awda na Indonesia bado umewekewa vikwazo vikali, huku kukiripotiwa uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu, mafuta na vitengo vya damu na operesheni za WHO zinaendelea kutatizwa kwa kiasi kikubwa.”

Amesema “tangu Oktoba 2023 na kufikia tarehe 4 Desemba mwaka huu asilimia 58 ya operesheni 273 zilizopangwa kuongozwa na WHO ndani ya Gaza aidha zilikataliwa, kufutwa au kuzuiwa, huku kukiwa na operesheni chache zaidi zinazokamilika Kaskazini mwa Gaza.”

Mashambulizi ya utawala haramu wa  Israel katika hospitali ya Kamal Adwan yanaendelea.

Dkt. Peeperkon ameeleza kuwa  tarehe 5 Disemba, ndege zisizo na rubani za jeshi la Israeli zilitekeleza shambulizi katika hospitali ya Kamal Adwan huko Beit Lahia. Kulingana na wizara ya afya ya Gaza mgonjwa mwenye umri wa miaka 16 aliuawa akiwa kwenye kitimwendo akipelekwa kwenye vipimo vya x-ray.

WHO inasema tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi 6 Desemba 2024, zaidi ya mashambulizi 1249 yametekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya huduma za afya ambapo mashambulizi 591 yamethibitishwa huko Gaza wakati  mashambulizi 658 yamefanyika katika Ukingo wa Magharibi.