Ufaransa; kuanzia mivutano hadi mgogoro wa kisiasa
Hatimaye wabunge wa vyama vya mrengo wa kulia na kushoto vyenye misimamo mikali katika bunge la taifa la Ufaransa wametimiza ahadi yao na kuiondoa madarakani serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Michel Barnier.
Kura ya kutokuwa na imani na serikali ya Michel Barnier iliyopigwa na wawakilishi wa bunge la taifa la Ufaransa imeakisiwa pakubwa ndani ya nchi hiyo na barani Ulaya kwa ujumla. Serikali ya Barnier iliyodumu kwa miezi mitatu tu ni serikali ya muda mfupi zaidi kuwahi kuhudumu huko Ufaransa tangu mwaka 1958.
Kuanzia mwaka 1962 pia hii ni mara ya kwanza kuona serikali ya Ufaransa inaondolewa madarakani kupitia wabunge kuipigia kura ya kutokuwa na imani nayo. Ufaransa pamoja na Ujerumani ni injini za Umoja wa Ulaya kwa sababu kila tukio lolote kubwa linajitokeza katika ngazi ya serikali mbili za nchi hiyo huambatana na radiamali na maoni tofauti kutoka Umoja wa Ulaya. Hivi sasa pia serikali za Ujerumani na Ufaransa zinakabiliwa na migogoro. Nchini Ujerumani Kansela wa nchi hiyo Olaf Scholz amepoteza wingi wa viti bungeni baada ya chama cha Free Democrats kujitoa katika serikali ya mseto kufuatia mvutano kuhusu kadhia ya bajeti ya nchi hiyo ya mwaka 2025 na kulazimika kutangaza uchaguzi wa mapema mwezi Januari mwakani.
Huko Ufaransa pia hali ya kisiasa inaendelea kuwa tata. Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron alidhani kuwa baada ya kushindwa vyama vya mrengo wa kati katika uchaguzi wa bunge la Ulaya angeweza kushinda na wingi kamili wa uwakilishi bungeni kwa kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge.
Rais wa Ufaransa alidhani kuwa baadhi ya kura za hapana zilizopigwa katika uchaguzi wa rais wa 2017 na 2022 kwa kumhofia Marine Le Pen, kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha National Front, zingejikariri pia katika uchaguzi wa mapema wa wabunge. Hata hivyo jambo hilo halijatokea kinyume na alivyofikiria Macron.
Chama cha siasa kali cha The National Rally kinachoongozwa na Marine Le Pen kilishinda viti 144 kati ya viti 577 vya Bunge la Taifa la Ufaransa na kushika nafasi ya tatu, lakini muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Macron pia viliambulia viti 162 kwa pamoja.
Muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto na vyenye misimamo mikali ulipata kura nyingi zaidi kwa kushinda viti 192 bungeni. Hatimaye, hakuna chama chochote kutoka muungano wa kushoto hadi vile vya mrengo wa kulia vyenye misimiamo mikali kilichoweza kupata ushindi wa wingi wa viti vya uwakilishi yaani kushinda viti vya bunge 288 kwa ajili ya kuunda serikali. Baada ya kura za bunge kugawanywa miongoni mwa vyama vyenye mielekeo mbalimbali Macroni alitaraji kuwa angefanikiwa kuiondoa Ufaransa katika hali ngumu kwa kumteuwa Michel Barnier mwanasiasa mkongwe kutoka mrengo wa kulia-kati kuwa Waziri Mkuu kuiongoza serikali baada ya miezi miwili ya mazungumzo na mashauriano. Hata wapinzani wa Macron wamepinga bajeti ya Barnier ya 2025 na kumpigia kura ya kutokuwa na imani na serikali yake.
Deni la serikali ya Ufaransa ni yuro trilioni 3.2. Migogoro mikubwa kadhaa, pamoja na janga la Uviko-19 na matatizo ya nishati yaliyosababishwa na vita Russia na Ukraine, pamoja na ukuaji wa kusuasua wa uchumi, mapato ya ushuru ya kiwango cha chini; yote hayo yameiweka Ufaransa katika hali ngumu. Hii ni katika hali ambayo makampuni mbalimbali ya Ufaransa yameanza kuwaachisha kazi wafanyakazi wake na hivyo kuwaweka katika hali ngumu. Wakati huo huo wanahisa na wamiliki wa hati fungani za serikali ya Ufaransa wanauza hisa na hati fungani zao. Kwa ufupi ni kuwa mwelekeo wa kiuchumi wa Ufaransa si mzuri. Macron ana machaguo machache ya kuondokana na hali ngumu ya kisiasa na kiuchumi inayomkabili.
Kuchagua mbadala wa Michel Barnier si kazi rahisi. Kwa upande mmoja, haiwezekani kufanya uchaguzi wa mapema hadi msimu ujao wa joto. Kwa kuzingatia hali ngumu anayopitia sasa Macron miongoni mwa fikra za waliowengi inatarajiwa kuwa uchaguzi huo utamalizika kwa manufaa ya vyama vinavyomuunga mkono. Yeyote atakayechaguliwa kuchukua nafasi ya Michel Barnier atakabiliwa na kibarua cha bajeti ya 2025.
Kama Macron pia atataka kufuata sera za Barnier ili kupunguza nakisi ya bajeti, atakabiliwa na hatima sawa na ya Barnier. Chaguo la Macron litakuwa ni kuchagua Mteknokrati asiyeegemea upande wowote kwa ajili ya nafasi ya Waziri Mkuu ambaye atakuwa na mamlaka madogo. Sasa hapa Rais Emmanuel Macron anapasa kutumia mamlaka maalum ya rais ili kutekeleza mpango wa bajeti ya mwaka ujao wa 2025. Chaguo la pili la Macron litakuwa ni kufikia mapatano na Marine Le Pen kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha National Front. Wakati huo huo vyama vya upinzani vinaona Macron anapasa kujiuzulu kama njia pekee ya kuiondoa Ufaransa katika mkwamo huu wa sasa. Hii ni katika hali ambayo imesalia miaka mitatu kabla ya kumalizika muhula wa urais wa Macron, ambaye anapinga vikali suala hili.
Ni wazi kuwa vutanikuvute ya kisiasa nchini Ufaransa imedhihirisha taathira zake ndani ya Umoja wa Ulaya khususan kuhusu suala la misaada ya kijeshi kwa Ukraine na namna ya kukabiliana na muhula wa pili wa urais wa Trump.