Takwa la Trump la kusitishwa mapigano mara moja nchini Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i119936-takwa_la_trump_la_kusitishwa_mapigano_mara_moja_nchini_ukraine
Katika ujumbe aliotoa baada ya kukutana na Volodymyr Zelenskiy na Emmanuel Macron, Marais wa Ukraine na Ufaransa mjini Paris, Donald Trump, rais mteule wa Marekani ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano nchini Ukraine.
(last modified 2024-12-09T23:17:51+00:00 )
Dec 09, 2024 23:17 UTC
  • Takwa la Trump la kusitishwa mapigano mara moja nchini Ukraine

Katika ujumbe aliotoa baada ya kukutana na Volodymyr Zelenskiy na Emmanuel Macron, Marais wa Ukraine na Ufaransa mjini Paris, Donald Trump, rais mteule wa Marekani ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano nchini Ukraine.

Akiashiria hasara ya mamia kwa maelfu ya wanajeshi na raia wa Ukraine tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine, Trump amesisitiza kuwa Zelensky yuko tayari kufanya mapatano ya kusitisha vita. Rais mteule wa Marekani ameandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Kusitishwa mapigano kunapaswa kuanza mara moja na mazungumzo yaanzishwe. Ikiwa vita vitaendelea, familia nyingi zitapoteza maisha. Ikiwa vita vitaendelea, vinaweza kugeuka kuwa kitu kikubwa na kibaya zaidi.“

Vita vya Ukraine ni mojawapo ya maswala muhimu yanayozingatiwa na Donald Trump, ambaye aliahidi kuvimaliza haraka katika hotuba zake nyingi za uchaguzi.

Trump alisema katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York mwezi Septemba kwamba: "Ninaamini ninaweza kufanikisha makubaliano haraka sana kati ya Rais Putin na Rais Zelensky. Kinachoendelea Ukraine ni fedheha; vifo vingi, uharibifu mwingi. Haya ni mambo ya kutisha, halafu unaona Marekani inalipa gharama zaidi."

Tangu kuanza vita nchini Ukraine, Marekani imetoa msaada wa kijeshi wa zaidi ya dola bilioni 62 kwa Ukraine, na msaada huu bado unaendelea, hivi kwamba wiki iliyopita, Rais wa Joe Biden wa Marekani, alitoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine wenye thamani ya dola milioni 988.

Trump, ambaye amekuwa akihubiri mara nyingi sera ya 'Marekani Kwanza', anakuchukulia kuendelea kuwepo Marekani nchini Ukraine na msaada wa kifedha na kijeshi kwa Zelensky kama upotezaji wa rasilimali ambazo zinapaswa kutumiwa ndani ya Marekani na kwa ajili ya raia wa nchi hiyo.

Trump akiwa na Marais wa Ukraine na Ufaranza mjini Paris

Katika hali hii, na sasa kutokana na matukio ya Syria, kwa mtazamo wa Trump, huu ndio wakati mwafaka wa kumaliza vita vya Ukraine na kutangazwa usitishaji mapigano. Kwa upande mmoja anajaribu kuonyesha kuwa Russia ni dhaifu na kwa upande mwingine, anazitishia Ulaya na NATO na kumuweka Zelensky chini ya mashinikizo ili akubali matakwa yake.

Trump anazungumzia usitishaji vita huku takriban asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine ikiwa chini ya udhibiti wa Russia, ambapo katika wiki za hivi karibuni Russia imezidisha mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.

Kuhusiana na hili, Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia kwa mara nyingine tena amesema kwamba Moscow ina masharti ya kadhaa ya kusimamisha vita, likiwemo hili la Ukraine kutokuwa mwanachama wa NATO na kusimamisha ushirikiano wake wa kijeshi na muungano huu wa kijeshi.

Ingawa kwa maneno yake mwenyewe, Donald Trump anaona kuwa inawezekana kufikia makubaliano na kusitisha mapigano haraka huko Ukraine, lakini nchi za Ulaya zinaona kuwa zitakuwa zimejidhalilisha iwapo zitakubali masharti ya Russia. Zinaamini kwamba iwapo Ukraine itatoka kwenye udhibiti wazo, Russia itasonga mbele hadi kwenye kitovu cha Ulaya, kwa hivyo, zina wasiwasi mkubwa kuhusiana na mustkbali wao. Kwa upande mwingine, ingawa viongozi wa Moscow wanakaribisha wazo la kuhitimisha vita nchini Ukraine, lakini hawaoni kuwa suala hilo linawezekana katika mazingira ya hivi sasa.

Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, ameashiria kwamba Moscow inakaribisha mazungumzo yenye nia njema na yanayozingatia kuheshimiwa maslahi ya pande mbili na kusema: Trump na timu yake wanatuma ishara za kutatanisha kuhusu suala hili kwa kuukejeli utawala wa sasa wa Marekani. Wanazingatia kanuni ya "Marekani Kwanza" na "Amani kwa kutumia Nguvu". Mtazamo huu ambao umejaa siasa za mabavu, hauendani na msimamo wa Russia. Inaonekana Trump anakabiliwa na hali ngumu ambayo kwa sasa anajaribu kuidhibiti kwa nara na matamshi matupu, lakini haionekani kuwa anaweza kumaliza vita vya Ukraine kupitia siasa hizi.