Trump asema kuna 'uwezekano mkubwa' atakata misaada kwa Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i119938-trump_asema_kuna_'uwezekano_mkubwa'_atakata_misaada_kwa_ukraine
Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema 'kuna uwezekano mkubwa' kuwa atapunguza misaada ya Washington kwa Ukraine mara tu atakapoingia madarakani.
(last modified 2024-12-09T23:18:27+00:00 )
Dec 09, 2024 23:18 UTC
  • Trump asema kuna 'uwezekano mkubwa' atakata misaada kwa Ukraine

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema 'kuna uwezekano mkubwa' kuwa atapunguza misaada ya Washington kwa Ukraine mara tu atakapoingia madarakani.

Trump ameyasema hayo katika mahojiano na chaneli ya NBC yaliyopeperushwa hewani saa chache baada ya kutoa wito wa 'kusitishwa mara moja mapigano' kati ya Russia na Ukraine.
 
Katika mahojiano hayo, Trump aliulizwa, kama Ukraine inapaswa kujiandaa kwa msaada mdogo kutoka kwa Marekani baada ya yeye kuapishwa mwezi ujao wa Januari, naye akajibu kwa kusema “inawezekana. Ndio, inawezekana sana, ni hakika".
 
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon mapema mwezi huu, Washington ilitenga dola bilioni 131.36 kwa ajili ya Ukraine tangu Februari 2022, lakini Taasisi ya Kiel ya Uchumi wa Dunia ya Ujerumani imesema, ni chini ya dola bilioni 90 tu kati ya hizo zimetolewa kupatiwa Ukraine.
 
Katika kipindi chote cha kampeni zake, Trump aliahidi mara kadhaa kwamba angemaliza mzozo wa Ukraine ndani ya "saa 24" baada ya kuchukua madaraka, bila kutoa maelezo maalumu kuhusu namna atakavyofanikisha suala hilo.
Hata hivyo, inaaminika kuwa atatumia kitisho cha kupunguzwa misaada ya Marekani ili kumshurutisha kiongozi wa Ukraine Vladimir Zelensky kufanya mazungumzo, na tishio la kuongeza misaada hiyo kumshinikiza Rais wa Russia Vladimir Putin akubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo.
 
Siku ya Jumamosi, Trump alikutana na Zelensky na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Paris kwa mazungumzo ya papo kwa papo ambayo inasemekana "alisita sita" kuhudhuria. Hata hivyo hakuna yeyote kati ya watatu hao aliyezungumza na waandishi wa habari kueleza yaliyozungumzwa kwenye mkutano huo uliochukua muda wa dakika 40.../