Umoja wa Mataifa wapasisha azimio la kusitishwa vita Gaza
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa wingi wa kura azimio la kutaka kusitishwa mara moja na bila masharti mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Wanachama 158 walipiga kura kuliunga mkono azimio hilo, tisa walilipinga na 13 walijizuia kupiga kura.
Azimio la kusitisha mapigano linachukuliwa kama ishara, kwani limekataliwa na Marekani na Israel.
Baraza hilo pia limeidhinisha azimio jengine linaloliunga mkono Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, apalestina 42 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya alfajiri ya jana yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Gaza.
Mwezi wa 14 wa mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza unamalizika, na mashambulizi ya mabomu katika maeneo tofauti ya Ukanda huo yanaendelea huku makumi ya wakazi wa Gaza wakiuawa shahidi na kujeruhiwa kila siku.
Kwa kukaribia msimu wa baridi kali, wasiwasi umeongezeka zaidi kwa sababu utawala wa Kizayuni unazuia kutumwa misaada ya kibinadamu hususan nguo za joto. Kwa kuwasili majira ya baridi, maisha yamekuwa magumu hasa kwa watu waliolazimika kuhama makazi yao na ambao wanaishi kwenye mahema.