Ukandamizaji mkubwa wa "uhuru" katika vyuo vikuu vya Marekani
Sanjari na kuendelea maandamano ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya Marekani kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina na kuwaunga mkono wakaazi wa Gaza, vitendo vya ukandamizaji vya serikali na polisi wa Marekani dhidi ya wanafunzi vimeshadidi na kuchukua wigo mpana zaidi.
Donald Earl Collins, profesa katika Chuo Kikuu cha Washington, amesisitiza katika makala yake inayozungumzia vitendo vya ukatili vya serikali ya Marekani na polisi dhidi ya wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina ambao wanaandamana katika vyuo vikuu mbalimbali vya nchi hiyo: Leo vyuo vikuu vya Marekani viko katika kilele cha ukandamizaji na mbinyo mkubwa.
Collins ameongeza kuwa: Katika majira ya machipuo mwaka jana wakurugenzi na wakuu wa vyuo vikuu vya Marekani waliwalazimisha maafisa wa kutekeleza sheria kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wanafunzi, maprofesa na wafanyakazi wao kwa tuhuma za kutoa wito wa kukomeshwa mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza na kusimamishwa upanuzi haramu wa ukaliaji mabavu dhidi ya ardhi za Wapalestina.
Hii ni katika hali ambayo, vyuo vikuu vingi pia vilikataa kutoa shahada za wanafunzi waliohitimu masomo wanaopinga Israel na vikachukua hatua ya kuwasimamisha, kuwafukuza au kutishia kuwafukuza wanafunzi kwa kosa eti la kushiriki katika maandamano ya kulaani jinai za Israel dhidi ya Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya Wapalestina na vile vile sisitizo la utawala wa Kizayuni la kuendeleza jinai zisizo na mfano dhidi ya Wapalestina kwa kuzuia njia za kupeleka misaada na dawa na chakula jambo ambalo limesababisha njaa katika ukanda huo ni mambo ambayo yameshadidisha wimbi la maandamano ya wanafunzi barani Ulaya na Marekani. Wimbi la maandamano hayo lilianza tangu kuanza kwa vita vya Gaza Oktoba mwaka jana (2023)
Katika miezi kadhaa iliyopita, wanafunzi wa mataifa tofauti ya Ulaya na Marekani wamesisitiza mara kwa mara juu ya udharura wa kusitishwa mapigano na kukomesha mauaji ya Wapalestina kwa kufanya maandamano. Hata hivyo kuendelea vita kumepelekea kushtadi pia maandamano ya wanafunzi, na ukandamizaji wa polisi dhidi ya wanafunzi wanaoandamana, kiasi kwamba, katika vyuo vikuu vingi vya Marekani, licha ya kauli mbiu zote za uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kujieleza au uhuru wa kusema, wanafunzi wengi wamekamatwa au kunyimwa fursa ya elimu, na mchakato huu unaendelea, na hii imezidi kuweka wazi kwamba, madai ya uhuru wa kutoa maoni na kutambuliwa kwake na Marekani na nchi nyingine za Magharibi na urongo mtupu..
Kwa hakika hali ya hivi sasa inaonesha kuwa, suala la uhuru linaruhusiwa tu na watawala wa nchi za Magharibi pale linapounga mkono siasa za Washington na waitifaki wake hususan utawala wa Kizayuni. Vinginevyo, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Licha ya ukandamizaji wote huo, lakini wanafunzi wa Marekani na Ulaya bado wanataka kukomeshwa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza, na maandamano yangali yanafanyika katika vyuo vikuu mbalimbali vya Marekani na Ulaya.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Kiebrania la Yediot Aharonot, hali hiyo imevifanya vyuo vikuu vya Marekani na Kanada kutia saini mikataba na makampuni ya ulinzi ya Israel au makampuni mengine ya ulinzi ambayo wanachama wake wamepewa mafunzo katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel), ili kukandamiza maandamano ya wafuasi wa Palestina katika vyuo vikuu hivyo.
Gazeti hili la Kiebrania limeandika: Baada ya Donald Trump kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani, ameahidi kuzipiga faini taasisi za kielimu ambazo kulingana na yeye, haziwashughulikii ipasavyo wale aliowaita kuwa "wendawazimu na wafuasi wa Hamas".
Ukweli wa mambo ni kuwa, hii sio mara ya kwanza kuchukuliwa hatua za ukandamizaji kama hizi dhidi ya wanafunzi nchini Marekani. Kwa hakika, licha ya kauli mbiu zote za hadaa za Marekani na washirika wake kuhusu kuheshimu na kuzingatia kwao haki ya uhuru, lakini kivitendo imekuwa na msimamo wa kindumakuwili. Lilo wazi na bayana ni kuwa, kila ambacho ni kinyume na sera na matakwa ya serikali ya Marekani na viongozi wa utawala wa Kizayuni kinahesabiwa kuwa ni mstari mwekundu na lazima kukabiliana nacho.
Joseph Massad, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Columbia, anaandika kuhusiana na hili ya kwamba: Vyuo vikuu na mfumo wa kiliberali na sheria zinazowaunga mkono hufanya kazi vizuri wakati uhuru wa kitaaluma na uhuru wa kujieleza haupelekea kuibuka upinzani dhidi ya hegemonia (mamlaka ya kutoa amri). Hii ina maana kwamba wakati utetezi wa uhuru unapopingana na hegemonia (mamlaka ya kutoa amri na kuamrisha) na kuwa tishio kwa itikadi inayotawala, huchukuliwa hatua mbalimbali za ukandamizaji ndani ya chuo kikuu na kwa nguvu za nje – iwe ni vyuo vikuu binafsi au vya umma.
Licha ya kuwa ukandamizaji na vitisho katika vyuo vikuu vya Marekani na Ulaya dhidi ya wafuasi wa Palestina unaendelea, lakini kwa mtazamo wa dhamiri zilizo hai kila mahali duniani, jinai za Israel haziwezi kupuuzwa na vitendo vya uadui haviwezi kuzima moto wa hasira za wapinzani wa utawala wa Kizayuni wa Israel.