Russia yamkamata mshukiwa 'aliyeajiriwa na Ukraine' kwa mauaji ya Jenerali Kirillov
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120306-russia_yamkamata_mshukiwa_'aliyeajiriwa_na_ukraine'_kwa_mauaji_ya_jenerali_kirillov
Mamlaka ya Russia inasema imemkamata mshukiwa anayehusika na mauaji ya Jenerali wa ngazi za juu, Igor Kirillov, ambaye alikuwa mkuu wa kitengo cha silaha za kemikali cha jeshi la nchi hiyo, na kuongeza kuwa aliajiriwa na Ukraine.
(last modified 2024-12-18T10:00:45+00:00 )
Dec 18, 2024 10:00 UTC
  •  Jenerali Igor Kirillov
    Jenerali Igor Kirillov

Mamlaka ya Russia inasema imemkamata mshukiwa anayehusika na mauaji ya Jenerali wa ngazi za juu, Igor Kirillov, ambaye alikuwa mkuu wa kitengo cha silaha za kemikali cha jeshi la nchi hiyo, na kuongeza kuwa aliajiriwa na Ukraine.

Memaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Russia, Irina Volk amesema mshukiwa huyo, raia wa Uzbekistan mwenye umri wa miaka 29, amekamatwa katika kijiji cha Chernoye katika wilaya ya Balashikha ya Moscow leo Jumatano.

Irina Volk amesema mshukiwa huyo ambaye jina lake halikutajwa, alidaiwa kuajiriwa na Huduma ya Usalama ya Ukraine (SBU) kutekeleza shambulio lililomuua Jenerali Igor Kirillov na msaidizi wake huko Moscow.

Uchunguzi umebaini kuwa mshambuliaji huyo alikuwa ameahidiwa dola 100,000 na kusafirishwa hadi Umoja wa Ulaya baada ya kufanikisha kazi yake.

Kamati ya uchunguzi imesema katika taarifa yake kwamba bomu lililokuwa limetegwa kwenye pikipiki iliyokuwa imeegeshwa kwenye lango la jengo la makazi ya watu huko Ryazansky Prospekt mjimi Moscow limeripuka mapema jana na kumuua Kirillov na msaidizi wake.

Msemaji wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Russia amesema, mshukiwa huyo amekiri kutega bomu hilo.