Wazayuni wa Uingereza wakosolewa kwa kupinga idadi ya waliouawa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120312-wazayuni_wa_uingereza_wakosolewa_kwa_kupinga_idadi_ya_waliouawa_gaza
Shirika moja lenye makao yake makuu nchini Uingereza linalofadhiliwa na lobi ya Wazayuni limekabiliwa na shutuma kali kutokana na ripoti yake ya hivi karibuni inayodai kwamba, idadi ya walioaga dunia kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza "imetiwa chumvi ili kuichafua Israel."
(last modified 2024-12-18T10:06:58+00:00 )
Dec 18, 2024 10:06 UTC
  • Wazayuni wa Uingereza wakosolewa kwa kupinga idadi ya waliouawa Gaza

Shirika moja lenye makao yake makuu nchini Uingereza linalofadhiliwa na lobi ya Wazayuni limekabiliwa na shutuma kali kutokana na ripoti yake ya hivi karibuni inayodai kwamba, idadi ya walioaga dunia kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza "imetiwa chumvi ili kuichafua Israel."

Jumuiya ya Henry Jackson Society (HJS), kikundi cha wasomi mashuhuri cha mrengo wa kulia, kinachojulikana kwa kuwa na chuki dhidi ya Uislamu na kinachotetea sera za kuingilia kijeshi katika nchi mbalimbali, kilidai kuwa Wizara ya Afya ya Gaza inazidisha na kutia chumvi takwimu za walioaga dunia kutokana na vita vya mauaji ya kimbari ya Israel ambayo yamekuwa yakiendelea kwa karibu mwaka mmoja na nusu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya Wapalestina 45,000 wameuawa tangu utawala wa Tel Aviv uanzishe vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo lililozingirwa, Oktoba 7, 2023.

Idadi kubwa ya waliouawa na Israel huko Gaza ni watoto na wanawake

Zaidi ya mauaji 9,000 yametekelezwa katika kipindi hicho cha miezi 14. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanakadiria idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi ya Israel kuwa ni kubwa zaidi huku makumi ya maelfu wakiwa wamekwama chini ya vifusi.

Waangalizi wa nyanjani na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa madai ya Henry Jackson Society (HJS), kwamba Wizara ya Afya ya Gaza inazidisha na kutia chumvi takwimu za walioaga dunia kutokana na vita vya mauaji ya kimbari ya Israel sio ya kweli na kwamba yanapuuza athari mbaya za vita vya mauaji ya halaiki ya Israel dhidi ya watu wa Gaza.

Wanasisitiza kuwa madai hayo ya HJS pia yanatumika kuuondoa hatiani na kuusafisha utawala wa Kizayuni wa Israel uliosababisha maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika zama za sasa.