Nchi mbalimbali zaikosoa Marekani kwa kuzuia usitishaji wa mapigano huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120374-nchi_mbalimbali_zaikosoa_marekani_kwa_kuzuia_usitishaji_wa_mapigano_huko_gaza
Mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambaye ndiye mkuu wa sasa wa baraza hilo, amekataa kujibu shutuma za wanachama wengine kuhusu kura mfululizo ya turufu ya nchi hiyo ya kuzuia usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, na badala yake amezishutumu nchi nyingine wanachama kwa kutokuwa na matumaini.
(last modified 2024-12-20T04:26:25+00:00 )
Dec 20, 2024 04:26 UTC
  • Baraza la Usalama la UN
    Baraza la Usalama la UN

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambaye ndiye mkuu wa sasa wa baraza hilo, amekataa kujibu shutuma za wanachama wengine kuhusu kura mfululizo ya turufu ya nchi hiyo ya kuzuia usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, na badala yake amezishutumu nchi nyingine wanachama kwa kutokuwa na matumaini.

Ni baada ya wawakilishi wa nchi mbalimbali duniani kulikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa sababu ya kuitisha mkutano wa kupitia upya hali ya Gaza, chini ya uenyekiti wa Marekani ambayo ni mpinzani mkuu wa usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Vassily Nebenzia, ​​Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, amesema kuwa hali ya Gaza imekuwa mbaya zaidi siku baada ya siku tangu mwaka jana, lakini licha ya hali hiyo, Merekani imepiga kura ya turufu dhidi ya maazimio kadhaa ya kusitisha mapigano katika eneo hilo.

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, Geng Shuang pia amesema kwamba juhudi za Baraza la Usalama za kumaliza mgogoro wa Gaza daima zimekuwa zikikwamishwa na mjumbe mmoja wa kudumu wa baraza hili, na Jumatano iliyopita Baraza Kuu la UN lilipasisha maazimio mawili ya kusitishwa vita mara moja huko Gaza na kuunga mkono Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), lakini katika wiki hii moja, mamia ya watu wameuawa shahidi huko Gaza.Gaza

Watoto na wanawake ndio wahanga wakuu wa ukatili wa Israel

Wakati huo huo, Riyad Mansour, mwakilishi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa zaidi ya Wapalestina 150,000 wa Ukanda wa Gaza wameuawa, kujeruhiwa au kulemazwa na mashambulizi ya Israel, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Ameongeza kuwa: "Baraza la Usalama limeshindwa kabisa kukabiliana na uhalifu huo, na kutokana na kura ya turufu ya mara kwa mara ya Marekani, maazimio yote ya kusitisha mapigano yamefeli.

Tangu mwaka 1970 hadi sasa, Marekani imetumia kura ya veto mara 49 katika Baraza la Usalama dhidi ya maazimio yanayohusiana na Israel, na la mwisho ni kura ya turufu ya serikali ya Washington dhidi ya rasimu ya azimio la kusitisha vita na mauaji ya kimbari huko Gaza.