Imethibitika: Gaidi aliyeua watu Ujerumani hana mfungamano na Uislamu
(last modified Sat, 21 Dec 2024 13:40:59 GMT )
Dec 21, 2024 13:40 UTC

Polisi ya Ujerumani imetangaza kuwa shambulizi soko la Krismasi huko Magdeburg halina mfungamano au msukumo wowote wa 'Kiislamu'.

Ni kufuatia shambulio la gari lililogonga umati wa watu kwenye soko la Krismasi katika mji wa Magdeburg nchini Ujerumani, jana Ijumaa.

Kwa mujibu wa tovuti ya T-Online, watu 11 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika hujuma hiyo.

Televisheni ya NTV imenukuu kauli ya mamlaka katika jimbo la shirikisho la Saxony-Anhalt kwamba "Dereva wa gari hilo aligonga umati wa watu kwenye soko la Krismasi huko Magdeburg, na kwamba ametiwa nguvuni.

Gaidi mzaliwa wa Saudi Arabia aliyehusika na shambulio la soko la Krismasi huko Magdeburg ametambuliwa kama Talib Al-Abdulmohsen.

 Talib ni Muislamu wa zamani anayeishi Ujerumani, na ni maarufu kwa machapisho yake ya mara kwa mara ya kupinga Uislamu na kutetea Uzayuni kwenye mitandao ya kijamii.

Jarida la Ujerumani Der Spiegel limeripoti kwamba mhalifu huyo ni daktari aliyebobea katika tiba ya kisaikolojia na anaunga mkono fikra za chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany.

Talib anatafutwa na Saudi Arabia kwa tuhuma zinazohusiana na ugaidi na biashara ya binadamu inayohusisha watu binafsi kutoka Saudi Arabia na mataifa mengine ya Ghuba ya Uajemi kelekea kwenye nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

 Ujerumani ilikataa kumrejesha Saudi Arabia na badala yake ikampa hifadhi ya kisiasa mwaka 2006.