China: Marekani inachezea moto na utaiunguza kwa kuizatiti kwa silaha Taiwan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120486-china_marekani_inachezea_moto_na_utaiunguza_kwa_kuizatiti_kwa_silaha_taiwan
China imeionya Marekani kuhusu hatua yake iliyochukua hivi karibuni zaidi ya kuipatia misaada ya kijeshi Taiwan na kusisitiza kwamba, kusaidia kile kiitwacho "uhuru wa Taiwan" kwa kuipa silaha Taipei ni sawa na kuchezea moto, na moto huo utaiunguza Marekani.
(last modified 2026-07-28T12:43:49+00:00 )
Dec 23, 2024 02:07 UTC
  • China: Marekani inachezea moto na utaiunguza kwa kuizatiti kwa silaha Taiwan

China imeionya Marekani kuhusu hatua yake iliyochukua hivi karibuni zaidi ya kuipatia misaada ya kijeshi Taiwan na kusisitiza kwamba, kusaidia kile kiitwacho "uhuru wa Taiwan" kwa kuipa silaha Taipei ni sawa na kuchezea moto, na moto huo utaiunguza Marekani.

Gazeti rasmi la serikali ya China la Global Times limeripoti kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imetoa indhari hiyo baada ya Ikulu ya White House kutangaza siku ya Ijumaa msaada zaidi wa kijeshi wa dola milioni 571.3 na kuidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya dola milioni 295 kwa Taiwan.
 
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema, Washington inakiuka kanuni ya China-Moja na taarifa tatu za pamoja zilizosainiwa na nchi hizo mbili.
 
"Kusaidia uhuru wa Taiwan kwa kuipa Taiwan silaha ni sawa na kuchezea moto na kutaifanya Marekani iungue; na kutumia suala la Taiwan ili kuidhibiti China ni jambo ambalo litafeli tu", amesisitiza msemaji wa wizara hiyo.
 
Beijing imeihimiza Washington mara kadhaa iache mara moja kuipatia Taiwan silaha na kuachana pia na hatua hatari zinazodhoofisha amani na utulivu katika Mlango-Bahari wa Taiwan.
 
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ametamka bayana: "tutachukua hatua zote za lazima ili kulinda kwa uthabiti mamlaka ya taifa ya kujitawala, usalama na umoja wa ardhi yetu".
 
Mapema mwezi huu, Marekani iliidhinisha pia mauzo ya silaha kwa Taiwan zenye thamani ya dola milioni 385.../