Kupanuka kundi la BRICS baada ya kujiunga nchi nyingine 13
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120606-kupanuka_kundi_la_brics_baada_ya_kujiunga_nchi_nyingine_13
Kundi la BRICS linaendelea kupanuka baada ya nchi nyingine 13 kujiunga na kundi hilo kama "washirika" kuanzia mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 26, 2024 00:41 UTC
  • Kupanuka kundi la BRICS baada ya kujiunga nchi nyingine 13

Kundi la BRICS linaendelea kupanuka baada ya nchi nyingine 13 kujiunga na kundi hilo kama "washirika" kuanzia mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu.

Yuri Ushakov, mshauri wa Rais wa Russia katika masuala ya sera za kigeni ambaye pia ni Mkuu wa Kamati ya Uratibu ya uongozi wa BRICS, amesema: Mialiko ya ushiriki wa nchi 13 zilizoomba uanachama imetolewa, na hadi sasa Belarus, Bolivia, Indonesia, Kazakhstan, Cuba, Malaysia, Thailand, Uganda na Uzbekistan zimethibitisha kupokea mialiko hiyo. Ameashiria namna Russia ilivyotekeleza wajibu wake kama mwenyekiti wa kundi hilo mwaka huu wa 2024 na kukubali kujiunga wanachama wapya katika muungano huo na kusema: Brazil itapewa uenyekiti wa kundi hilo kuanzia Januari Mosi 2025. Kama walivyotangaza viongozi wa Russia kabla ya Mkutano wa Kazan, maombi 35 ya kujiunga na BRICS yalipokelewa rasmi, huku nchi 13 zikikubaliwa kujiunga kama washirika. 

BRICS ni jumuiya ya kisiasa na kiuchumi, inayojumuisha mataifa yenye nguvu na uchumi unaoibukia duniani, ambayo ilianzishwa mwaka 2009. Jumuiya hiyo iliasisiwa ili kukabiliana na hatua za kujitanua na udhibiti wa nchi za Magharibi, hususan kwa uchumi wa dunia. Jumuiya hii iliundwa kwa ubunifu wa China na Russia pamoja na India, Brazil na Afrika Kusini na kisha ikapanuka kwa kujiunga Iran, Misri, Ethiopia na Imarati. 

BRICS na hatua za kuachana na sarafu za dola 

Kwa mtazamo wa kiuchumi, wanachama wa BRICS wanakusudia kukabiliana na udhibiti wa sarafu ya dola ya Marekani juu ya uchumi wa dunia, kushirikishwa mataifa yanayoibukia kiuchumi katika usimamizi wa uchumi wa dunia, na ushindani mkabala  wa nchi za Magharibi. Nchi za BRICS zinazozalisha zaidi ya robo ya utajiri wa dunia na zinaunda asilimia 42 ya jamii ya watu wote duniani, zinataka kuwepo uwiano wa kisiasa na kiuchumi duniani hasa mkabala wa Marekani na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya; Kwa msingi huo, nchi hizo zinatilia maanani suala la kuimarisha na kupanua mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kati ya wanachama wa BRICS, na kufanya miamala ya biashara kwa kuzingatia sarafu ya pamoja ya nchi wanachama.

Kuhusiana na suala hili, hivi karibuni nchi hizo zilipendekeza kuanzishwa sarafu mpya ya kidijitali au kutumia kapu la ubunifu la sarafu za BRICS katika miamala ya biashara. Kwa hakika udhibiti wa sarafu ya dola kwa uchumi wa dunia na pia hatua ya Marekani ya kutumia sarafu hiyo kama wenzo wa kisiasa dhidi ya nchi nyingine zinazokwenda kinyume na matakwa na maslahi ya Washington, vimepelekea kuongezeka nchi zinazotaka kujiunga na kundi la BRICS. 

Kwa miongo kadhaa sasa, Marekani inatumia sarafu ya dola kama silaha kuzishinikiza nchi ambazo haziendani na malengo na matakwa yake. Katika uwanja huu tunaweza kuashiria vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran, Russia, Venezuela na Cuba.

Kadhia hii imepata umuhimu mkubwa hivi sasa baada ya kuchaguliwa Donald Trump kuwa Rais wa Marekani. Trump hivi karibuni alizitishia nchi wanachama wa kundi la BRICS kwamba ataongeza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa za nchi hizo iwapo zitachukua hatua ya kuweka kando sarafu ya dola. Trump aliandika katika mtandao wa kijamii wa Truth kwamba: "Nchi wanachama wa BRICS zinapasa kuahidi kwamba hazitaanzisha sarafu mpya ya kundi hilo na wala hazitaunga mkono matumizi ya sarafu nyingine mkabala wa dola ya Marekani; la sivyo zitaainishiwa ushuru wa kiwango cha juu na zitalazimika kuachana na soko la Marekani." Matamshi haya ya Rais mteule wa Marekani yanaonyesha kuwa udhibiti wa sarafu ya dola duniani unakabiliwa na tishio kuu kutoka kundi la BRICS. 

Jeffrey Sachs profesa wa Chuo Kikuu cha Columbia na Mkurugenzi wa Taasisi ya Earth Institute anasema: "Marekani imebadili uga wa uchumi wa kimataifa kuwa uwanja wa kijeshi, hasa kwa kutumia sarafu ya dola kama silaha.

Jeffrey Sachs, Mkurugenzi na Profesa wa Chuo Kikuu cha Columbia 

Katika mazingira haya, kundi la BRICS limechukua hatua nyingine ambazo hazikuwa aina fulani ya mlingano wa kijiografia dhidi ya ukandamizaji na hatua za kujitanua za Marekani pekee, bali kama hitajio la kiutendaji la kutafuta njia mbadala za kufanya biashara baina ya nchi wanachama. Takwimu za mabadilishano ya kibiashara na mipango ya nchi wanachama wa BRICS zinaonyesha kuwa, taasisi hiyo ina uwezo mkubwa sana kuelekea ustawi wa haraka wa kiuchumi na kuwa kambi athirifu yenye ushawishi na maamuzi katika uchumi wa kimataifa huku ikipiga hatua siku baada ya siku.