Malalamiko ya wananchi wa Pakistan kwa kuendelea ukosefu wa amani Parachinar
Vyama na makundi ya kidini ya Waislamu wa Kishia yamefanya maandamano katika miji tofauti ya Pakistan ikiwemo ya Islamabad na Karachi kulaani na kulalamikia kuendelea ukosefu wa amani katika mji wa Parachinar na jinai zinazofanywa na magenge ya kigaidi na ya ukufurishaji katika eneo hilo.
Wananchi wa Pakistan wamelalamikia vikali jinsi serikali na taasisi za usalama za nchi hiyo zinavyopuuza kutekeleza wajibu wao wa kuimarisha haraka usalama katika mji wa Parachinar na kuwatia mbaroni magaidi wanaofanya jinai mjini humo, na wameitaka serikali ya shirikisho pamoja na serikali ya jimbo la Kheybar kuchukua hatua za haraka za kuwadhaminia usalama wananchi wa Parachinar.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, waziri wa mambo ya ndani wa Pakistan alipotembelea eneo hilo alitilia mkazo wajibu wa kuimarishwa haraka usalama katika mji wa Parachinar, kuondolewa mzingiro na kufunguliwa njia za kuunganisha mji huo na maeneo mengine.
Wakazi wa mji wa Parachinar wanateseka kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na uhaba wa dawa na chakula kutokana na kuzingirwa mji huo na kukatwa mawasiliano baina yake na maeneo mengine ya Pakistan kwa karibu miezi mitatu sasa. Wananchi wa mji huo wamekuwa wakilalamika sana, lakini malalamiko yao yalikuwa hayafiki mbali, hivyo makundi na vyama vingine kikiwemo Chama cha Baraza la Umoja wa Waislamu, wameamua kuitisha maandamano ya miji yote ya Pakistan ili kufikisha kwa walimwengu kilio cha wananchi wa mji wa Parachinar.
Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Hamid Hussein, mbunge wa Bunge la Taifa la Pakistan kutoka Chama cha Baraza la Umoja wa Waislamu akailaumu vikali serikali ya jimbo la Kheybar kwa kuzembea kutatua mgogora wa Parachinar na kuwapunguzia mateso wananchi wa mji huo; akitaka kuchukuliwe hatua kali na vyombo vya usalama vya Pakistan ikiwa ni pamoja na kuadhibiwa magaidi waliowaua kwa umati Waislamu wa Kishia mjini humo.
Malalamiko dhidi ya utendaji mbovu wa tawala za majimbo na serikali ya shirikisho na kushindwa kwao kutatua matatizo ya wananchi wa mji wa Parachinar yameongezeka katika hali ambayo Waziri Mkuu wa Pakistan, Shabhaz Sharif hivi karibuni alitoa amri ya kupelekwa haraka dawa na chakula cha dharura kwa wananchi wa Parachinar. Alifikia hata kuamrisha helikopta kadhaa ziwachukkue wagonjwa wa mji wa Parachinar na kuwahamishia kwenye miji mingine kama Peshawar na Islamabad. Lakini pamoja na hayo, inaonenaka serikali ya shirikisho ya Pakistan haina haraka ya kutatuwa matatizo ya wananchi wa mji wa Parachinar. Upuuzaji wa serikali ya shirikisho ya Pakistan umeyafanya magenge ya kigaidi yaendelee kuwatesa na kuwakosesha amani na utulivu wananchi wa mji huo ambao asilimia kubwa ni Waislamu wa Kishia.
Tukumbuke kuwa takriban mwezi mmoja uliopita, magaidi wakufurishaji walivamia viunga vya mji wa Parachinar na kuua kwa umati zaidi ya Waislamu 50. Vikosi vya usalama vya Pakistan vilitumia suala hilo kufunga njia zote za kuingia na kutoka mjini humo na matokeo yake ni kuteseka wananchi wa Parachinar na kuongezeka sana matatizo yao.
Vyama vya Kishia vya Pakistan vinayalaumu magenge ya ukufurishaji kwa kutenda jinai za kutisha dhidi ya wananchi wa mji wa Parachinar. Vyama hivyo vinasisitiza kuwa lengo la magenge hayo ya kigaidi na ukufurishaji ni kuvuruga kabisa hali ya utulivu na amani na kushadidisha utengano katika safu za Waislamu.
Kwa kuzingatia yote hayo, kinachotarajiwa kutoka kwa serikali ya Pakistan ni kuimarisha haraka usalama katika mji wa Parachinar, kuwatia mbaroni na kuwaadhibu magaidi waliofanya jinai dhidi ya wananchi wasio na ulinzi na pia kuchukua hatua za haraka za kutatua masuala mengine ya wananchi ikiwa ni pamoja na kufungua njia za kuingia na kutoka mjini humo. Makundi na vyama vya Kishia vinasema kuwa, kuendelea serikali ya Pakistan kupuuza kutekeleza wajibu wake wa kuwadhaminia usalama wananchi wa mji wa Parachinar hakuna matunda mengine ila kufanikisha malengo ya watu ambao wanafurahi kuona wananchi Waislamu wa mji huo wanazidi kuteseka.