Kwa nini chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) inaongezeka nchini Uingereza?
Takwimu zilizochapishwa hivi karibuni nchini Uingereza zinaonyesha ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo.
Ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza inaonyesha kwamba kumekuwapo ongezeko la kutisha la uhalifu wa chuki uliolenga wafuasi wa dini makhsusi katika nchi hiyo. Kwa mujibu wa takwimu hizo, karibu 42% ya uhalifu wote uliorekodiwa katika eneo hili umetendwa dhidi ya Waislamu, hilo likiwa ongezeko la takriban 18-20% ikilinganishwa na mwaka jana (2023).
Hata hivyo ripoti za mashirika yasiyo ya kiserikali na watetezi wa haki za binadamu zinaonyesha ongezeko kubwa zaidi la chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo kiliko takwimu zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza. Shirika lisilo la kiserikali la "Tell MAMA" limetangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba mashambulizi ya maneno na vitisho katika anga ya mtandao yameongezeka kwa takriban 30% katika mwaka uliopita. Shirika hilo limekuwa likifuatilia kitaalamu rekodi za matukio ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza. Tell Mama imesema kwenye tovuti yake kwamba matukio mengi kati ya hayo yameripotiwa kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, X (zamani Twitter), Instagram na TikTok.
Kamisheni ya Haki za Kibinadamu ya Kiislamu (IHRC) pia ilitangaza katika uchunguzi wa hivi karibuni kwamba: Uingereza inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika uwanja wa ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu miongoni mwa nchi za Ulaya. Katika utafiti huo, zaidi ya 75% ya Waislamu waliohojiwa walisema kwamba walikumbana na ubaguzi au mienendo ya kudhalilishwa kwa uchache mara moja katika mwaka uliopita. 40% pia wamekiri kwamba mienendo hiyo ilikuwa mibaya sana kiasi kwamba, ilizidisha hisia za kutokuwa na usalama wa kibinafsi. Wanaharakati wa masuala ya kiraia wanataja mambo kadhaa kuhusiana na sababu za kushamiri chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza. Miongoni mwa mambo hayo ni hali iliyojitokeza katika jamii kutokana na matamshi ya kichochezi ya baadhi ya wanasiasa na mijadala yenye mwelekeo maalumu ya upande mmoja ya vyombo vya habari. Waziri wa zamani wa elimu wa Uingereza, Michael Gove, alisema katika mjadala uliozungumzia siasa kali kwamba "Uislamu wa kisiasa ni virusi” na akakwepa kujibu swali kuhusu hatua ya chama cha Conservative ya kukubali ufafanuzi wa chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).
Matokeo ya mienendo kama hii ni kwamba, kuna makundi ya watu katika jamii ya Waingereza wanaona kuwa ubaguzi dhidi ya Waislamu unaweza kuhalalishwa au hata kutambuliwa kuwa ni hatua ya kulinda utambulisho wa taifa!
Chuki na propaganda chafu dhidi ya Uislamu vimekuwa sera ya kimkakati ya serikali ya London. Katika kipindi cha miaka 14 ya utawala wake, serikali ya zamani ya kihafidhina ya Uingereza iliwaajiri watu waliokuwa wakipiga vita Uislamu na kueneza chuki dhidi ya Waislamu. Serikali ilipasisha sheria zinazowabana wahajiri na hivyo kivitendo ikawa inaendeleza sera ya kubana shughuli na harakati za kijamii za Waislamu wa Uingereza.
Baada ya kushika madaraka serikali ya chama cha Leba, kiwango cha chuki dhidi ya Uislamu hakijapungua, bali takwimu zinaonyasha kuwa kimeongezeka. Julai mwaka huu, Uingereza ilikuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye siasa kali za mrengo wa kulia na ya kibaguzi dhidi ya Waislamu na maeneo ya Kiislamu kwa wiki kadhaa.
Mwishoni mwa mwezi Julai, miji mbalimbali ya Uingereza ilikumbwa na maandamano makubwa baada ya kijana mwenye umri wa miaka 17 kushambulia karamu iliyohudhuriwa na watoto katika jiji la Southport. Watoto watatu waliuawa, na wengine kadhaa wakiwemo watu wazima wawili, walipelekwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya baada ya kujeruhiwa kwa kudungwa kisu.
Mara tu baada ya tukio hili, habari za uwongo zilichapishwa katika vyombo vya habari vya Uingereza kwamba mshambuliaji huyu alikuwa Mwislamu. Wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia walitumia habari hiyo ya uongo kama kisingizio na wakashambulia Waislamu na maeneo yao. Baadaye, gazeti la The Times limeripoti kwamba, tovuti ya "Channel 3 Now," ilichapisha habari feki na ya kupotosha mtandaoni ambayo ilimhusisha kwa uongo muomba ukimbizi bandia na tukio la kuchomwa visu watoto hao watatu.
Kwa upande wake, televisheni ya BBC News wa Uingereza umeripoti kuwa mshukiwa wa mauaji hayo ni mzaliwa wa Cardiff kwa wazazi wenye asili ya Rwanda na alihamia eneo la Southport mwaka 2013 na wala si mhajiri Muislamu muomba hifadhi kama ilivyodaiwa.
Mashambulizi yaliyowalenga Waislamu, misikiti, shule na vituo vya Waislamu nchini Uingereza wakati huo yalizua hofu na wasiwasi miongoni mwa Waislamu.
Watu mashuhuri wa Kiislamu wa Uingereza kama Humza Yousaf, aliyekuwa Waziri wa Kwanza wa Scotland na Sadiq Khan, Meya wa London, hawakuficha hofu na wasiwasi huo. Alipoulizwa iwapo anajisikia salama kama mwanasiasa Muislamu, Sadiq Khan alijibu, "Ni wazi, siko salama, ndiyo maana ninaishi kwa ulinzi wa polisi wa saa 24." Tangu alipochaguliwa kuwa Meya wa Landon mwaka wa 2016, Khan amepokea vitisho vingi na anasema timu ya polisi ya wanachama 15 ina jukumu la kumlinda yeye na familia yake. Mkewe, Sadia Ahmed, wakili mwenye asili ya Pakistani, pamoja na binti zao, Anisa na Amara, wanalindwa na polisi.
Kwa upande wake, Humza Yousaf, waziri wa zamani wa kwanza wa Scotland, alisema katika mahojiano na Telegraph kwamba, yeye na raia wengine wa makundi ya wachache wanahisi kwamba "Uingereza wao unatiliwa shaka." Humza Yousaf aliongeza kuwa: Hujuma dhidi ya Uislamu na wahamiaji imekuwa jambo "la kawaida" nchini Uingereza.
Wakati watu mashuhuri wa Kiislamu nchini Uingereza wanapoelezea hofu na wasiwasi kuhusu maisha nchini humo, hapana shaka kuwa hali itakuwa ngumu na ya kutia wasiwasi zaidi kwa Waislamu wa kawaida walio wachache, hasa wahamiaji na Waingereza wenye asili ya mataifa mengine.