Idadi ya watu wasio na makazi nchini Marekani yazidi kuongezeka
Idadi ya watu wasio na makazi nchini Marekani inazidi kuongezeka huku serikali ya nchi hiyo ikiendelea kutoa misaada ya silaha na zana za kijeshi kwa Israel inayofanya mauaji ya kimbari dhidi ya wakazii wa Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Nyumba na Ujenzi wa Miji ya Marekani imetangaza katika taarifa yake: Kufuatia mzozo wa ukosefu wa nyumba za bei nafuu, kupanda kwa mfumuko wa bei na kutokuweko ongezeko la kutosha la mishahara, idadi ya watu wasio na makazi nchini humo imefikia 771,480.
Taarifa ya Wizara ya Nyumba na Ujenzi wa Miji ya Marekani imeeleza kuwa, idadi ya watu wasio na makazi nchini Marekani imefikia rekodi ya kihistoria.
Kadhalika taarifa hiyo imeongeza kuwa, wakati idadi ya watu wasio na makazi nchini humo ilifikia zaidi ya watu 650,000 mnamo Januari 2023, idadi hii imefikia watu 771,480 mnamo Januari mwaka huu 2024 na hilo ongezeko la zaidi ya 18%.
Kwa mujibu wa wizara hiyo pamoja na mambo kama vile mgogoro wa nyumba za gharama nafuu, kupanda kwa mfumuko wa bei na ongezeko lisilo la kutosha la mishahara nchini Marekani, mgogoro wa afya na majanga ya kimaumbile pia yameathiri ongezeko la idadi ya watu wasio na makazi katika nchi hii.
Serikali ya Marekani ilitangaza hapo kabla katika ripoti yake kwamba kutokana na kupanda kwa bei ya nyumba na kupunguzwa kwa misaada wakati wa Corona, idadi ya watu wasio na makazi nchini imefikia kiwango cha juu zaidi tangu 2007 na kuanza kukusanya takwimu za watu wasio na makazi.
Marcia Fudge, Waziri wa Makazi na Maendeleo ya Miji wa Marekani aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter) kwamba data hizi zinaonyesha hitajio la dharura la suluhu na kwamba kusiwe na ukosefu wa makazi nchini Marekani.