Ndege ya Korea Kusini yaanguka na kuua watu 124
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120752-ndege_ya_korea_kusini_yaanguka_na_kuua_watu_124
Kwa akali watu 124 wamefariki dunia katika ajali ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan katika Mkoa wa Jeolla Kusini nchini Korea Kusini.
(last modified 2024-12-29T04:20:21+00:00 )
Dec 29, 2024 04:20 UTC
  • Ndege ya Korea Kusini yaanguka na kuua watu  124

Kwa akali watu 124 wamefariki dunia katika ajali ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan katika Mkoa wa Jeolla Kusini nchini Korea Kusini.

Vyanzo vya ndani vinaripoti kuwa, hadi sasa watu 124 wamethibiitishwa kuaga dunia katika ajali hiyo ya ndege ya abiria.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, watu wote waliokuwamo ndanii ya ndege hiyo wameaga dunia isipokuwa watu wawili.

Ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Bangkok, iliacha njia na kugongana na uzio wakati wa kutua.

Shirika la Habari la Yonhap limetangaza kuwa, ndege hiyo ya abiria iliacha barabara ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege wa Moan (kusini-magharibi mwa Korea Kusini) na kugongana na uzio wa uwanja huo na kisha kuwaka moto.

Kwa mujibu wa Shirika la Usalama wa Anga la Korea Kusini, ndege iliyopata ajali ilishika moto baada ya tatizo kutokea katika matairi yake.

Ajali hii si ya kawaida kwa Korea Kusini, ambayo imekuwa na rekodi nzuri ya usalama wa ndege katika miaka ya hivi karibuni.

Ikiwa idadi ya vifo itathibitishwa, hii itakuwa ajali mbaya zaidi ya ndege kuwahi kutokea katika ardhi ya Korea Kusini.