Mahakama ya Korea Kusini yatoa kibali cha kukamatwa kwa Yoon
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120828-mahakama_ya_korea_kusini_yatoa_kibali_cha_kukamatwa_kwa_yoon
Mahakama ya Korea Kusini imetoa waranti ya kukamatwa Rais wa nchi hiyo anayeandamwa na Bunge, Yoon Suk-yeol kutokana uamuzi wake wa kutangaza sheria ya kijeshi mnamo Desemba 3.
(last modified 2024-12-31T04:11:50+00:00 )
Dec 31, 2024 04:11 UTC
  • Yoon Suk-yeol
    Yoon Suk-yeol

Mahakama ya Korea Kusini imetoa waranti ya kukamatwa Rais wa nchi hiyo anayeandamwa na Bunge, Yoon Suk-yeol kutokana uamuzi wake wa kutangaza sheria ya kijeshi mnamo Desemba 3.

Mahakama ya Wilaya ya Seoul Magharibi mapema leo Jumanne imedhinisha hati hiyo kufuatia ombi la Makao Makuu ya Upelelezi wa Pamoja, ambayo inamchunguza kiongozi huyo wa Korea Kusini kutokana na kusababisha machafuko na matumizi mabaya ya madaraka.

Hatua hiyo ni mara ya kwanza kwa mamlaka kutaka kumweka kizuizini Rais aliyeko madarakani nchini Korea Kusini.

Kibali cha  sasa cha kukamatwa kinaweza kutumika hadi Januari 6, na mara amri hiyo itakapotekelezwa, Yoon atazuiliwa katika gereza jijini Seoul.

Yoon amekataa wito wa wapelelezi kuhojiwa mara tatu tangu kutangazwa kwa sheria ya kijeshi  Desemba 3.

Yoon anakabiliwa na uwezekano wa kufungwa jela maisha, au hata hukumu ya kifo, kutokana na utangazaji wake wa sheria ya kijeshi mnamo Desemba 3, ambao ililiitumbukiza taifa hilo la Asia Mashariki katika mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa katika miongo kadhaa.