Zaidi ya Warohingya 200 wakimbilia pwani ya Indonesia kwa boti mbovu
Zaidi ya Warohingya 200 wamewasili kwenye ufuo wa mkoa wa Aceh nchini Indonesia, katika wimbi jipya la kuhama makwao Waislamu hao walio wachache nchini Myanmar ambao wanakabiliwa na mateso na mauaji ya kimbari.
Afisa wa Indonesia amesema kwamba zaidi ya wakimbizi 200 wa Rohingya wamewasili katika pwani ya jimbo la Aceh, huku kukiwa na ongezeko la wakazi wasio na utaifa wanaowasili kwa njia ya bahari.
Mkuu wa wavuvi wa Aceh amesema kuwa zaidi ya wakimbizi 200 wa Rohingya waliwasili Jumapili, katika eneo la Magharibi Burulak katika kisiwa cha Sumatra, upande wa magharibi wa Indonesia.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi zinaonyesha kuwa zaidi ya wakimbizi 500 wa Rohingya waliwasili Indonesia kwa boti kati ya Oktoba na Novemba mwaka jana.
Afisa wa Kamisheni Mkuu ya Umoja wa Mataifa ya Kuhudumia Wakimbizi, (UNHCR) Faisal Rahman, amesema kuwa shirika hilo linaratibu na mamlaka za mitaa, na kwamba timu yake ingeelekea Burulak Magharibi jana Jumatatu.
Kwa miaka mingi, Warohingya wamekuwa wakiikimbia Myanmar, ambako wamekuwa wakidhulumiwa na kunyimwa uraia, mara nyingi wakisafiri kwa boti hatarishi kwa maisha yao wakitoroka mauaji yanayofanywa na Mabidha, au kutoka kwenye kambi katika nchi jirani ya Bangladesh, ambako karibu Warohingya milioni moja wamekimbilia.
Waislamu waliowachache wa Rohingya wamekuwa wakikandamizwa na jeshi na wanamgambo wa Kibudha nchini Myanmar tangu mwaka 2017, na wanatambuliwa kuwa ni wavamizi wa kigeni kutoka Asia Kusini.