Ripoti: Uhalifu wa kibaguzi umevunja rekodi nchini Ujerumani
Ujerumani imerekodi zaidi ya uhalifu 33,000 wa kibaguzi mwaka uliomalizika majuzi wa 2024, ambayo ni rekodi isiyo na kifani tangu mwanzo wa kusajili uhalifu huo mnamo 2001.
Takwimu zinaonyesha kuwa, uhalifu mwingi uliorekodiwa nchini Ujerumani ulikuwa katika muktadha wa propaganda na uchochezi wa chuki.
Hadi Novemba 30, 2024, polisi wa Ujerumani walirekodi jumla ya uhalifu 33 elfu 963 unaohusishwa na makundi ya mrengo wa kulia, ambapo elfu 1,136 ulikuwa uhalifu wa kutumia mabavu na ukatili, na asilimia kubwa iliandamana na kusababisha majeraha ya mwili.
Katika upande wa uhalifu uliochochewa kisiasa, takwimu zinaonyesha kuwa mnamo 2023, idadi ya uhalifu uliokithiri wa mrengo wa kulia uliweka rekodi mpya nchini Ujerumani, na jumla ya uhalifu 28,945 ulirekodiwa. Takwimu zinaonyesha kuwa uhalifu huo umeongezeka kwa asilimia isiyopingua 17.34 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.
Martina Reiner, mbunge wa Bunge la Ujerumani kutoka chama cha mrengo wa kushoto ametaja takwimu mpya za ukatili wa kibaguzi nchini humo kuwa ni za kutisha na kusema kuwa, wengi kati ya wanaofanya vitendo vya ukatili ni watu wazima, lakini pia kuna ongezeko la idadi ya vijana wanahusika na uhalifu huo.
Katika miaka ya karibuni, Ujerumani imeshuhudia ongezeko la ubaguzi wa rangi unaochochewa na vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia, kikiwemo chama cha siasa kali cha Alternative for Germany (AfD), ambacho kimekuwa kikitumia vibaya suala la mgogoro wa wakimbizi.