Hasara za moto huko Los Angeles zinakadiriwa kuwa dola bilioni 150
Kampuni ya huduma ya utabiri wa hali ya hewa ya Marekani imetangaza kwamba moto wa Los Angeles ni mojawapo ya majanga yaliyosababisha hasara kubwa zaidi katika historia ya Marekani, na kwamba kiasi cha uharibifu kinazidi dola bilioni 150.
Ripoti iliyotolewa na shirika la huduma ya utabiri wa hali ya hewa la Marekani, AccuWeather, inaonyesha kuwa uharibifu uliosababishwa na moto wa Los Angeles unaweza kuwa kati ya dola bilioni 135 na bilioni 150, suala linaloonyesha athari kubwa zilizotokea katika eneo lenye makazi na nyumba za gharama kubwa zaidi nchini Marekani.
Hapo awali, maafisa wa serikali ya Merekani walikadiria hasara iliosababishwa na moto wa Los Angeles kuwa ni dola bilioni 57.
Inakadiriwa kuwa, moto wa Los Angeles ni mojawapo ya majanga yaliyosababisha hasara kubwa zaidi katika historia ya Marekani. Mamlaka ya jiji la Los Angeles imetangaza katika takwimu za hivi karibuni kwamba majengo mengine 58,000 yanakabiliwa na hatari ya kuteketezwa kwa moto, na watu 153,000 wameagizwa kuhama.
Licha ya juhudi zinazoendelea kudhibiti moto huo, kiwango kamili cha uharibifu bado hakijajulikana, na Jonathan Porter, mtaalamu mkuu wa hali ya hewa katika AccuWeather, ameyataja maafa hayo kuwa mojawapo ya majanga yenye hasara kubwa zaidi ya moto katika zama za sasa.