Walimwengu waendelea kuandamana kuunga mkono Palestina
Maandamano ya kuunga mkono wananchi wa Palestina na kulaani jinai za utawala haramu wa Israel yameendelea kushuhhudiwa katika pembe mbalimbali duniani.
Muungano wa "Tunisia kwa ajili ya Kulinda Haki za Wapalestina" umefanya maandamano katika kuendeleza uungaji mkono na mshikamano wa kimataifa na Wapalestina na wafanyakazi wa matibabu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza uungaji mkono wao katika kukabiliana na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni.
Mbali na Tunisia kumeshuhudiwa pia maandamano ya wananchi wa Morocco kuunga mkono Palestina, uungaji mkono wa wanafunzi wa Uturuki kwa Gaza na maandamano ya Ujerumani dhidi ya mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa Kizayuni.
Aidha maandamano mengine ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina yameshuhudiwa nchini Uingereza, Jordan, Bahrain na katika mataifa mengine.
Kadhalika Yemen imeshuhudia maandamano makubwa ya mamilioni ya watu ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kulaani jinai za utawala haramu wa Israel.
Wakati huo huo, maandamano kama hayo yameshuhudiwa nchini Ireland. Waandamanaji nchini humo wamekosoa vikali sera za serikali ya Marekani na madola ya Magharibi kwa ujumla ya kuusaidia utawala vamizi wa Israel unaofanya mauaji kila uchao dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Washiriki wa maandamano hayo, huku wakitangaza mshikamano na taifa la Palestina, wametoa mwito wa kuendelea kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na kulaani vikali kulengwa kwa wafanyakazi wa sekta ya tiba na waandishi wa habari huko Gaza.