Jahanamu isiyo na mwisho huko Marekani; Moto unaendelea kuitafuna Los Angeles
https://parstoday.ir/sw/news/world-i121330-jahanamu_isiyo_na_mwisho_huko_marekani_moto_unaendelea_kuitafuna_los_angeles
Idadi ya watu waliopoteza maisha katika janga la moto ulioukumba mji wa Los Angeles nchini Marekani imeongezeka.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jan 12, 2025 04:29 UTC
  • Jahanamu isiyo na mwisho huko Marekani; Moto unaendelea kuitafuna Los Angeles

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika janga la moto ulioukumba mji wa Los Angeles nchini Marekani imeongezeka.

Mamlaka za tawala za mitaa katika mji wa Los Angeles zimetangaza kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha katika moto mkubwa ulioteketeza maeneo tofauti ya mji huo imeongezeka hadi watu 16 huku majengo elfu 12 yakiungua kikamilifu.

Shirika la habari la CBS News la Marekani limeripoti kuwa, moto ulioenea katika eneo la Los Angeles umeteketeza kikamilifu baadhi ya vitongoji na kuwalazimisha makumi ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Idara ya Taifa ya Hali ya Hewa imeonya kuwa hatari ya moto bado itaendelea kuwepo katika maeneo yote ya Los Angeles na Ventura hadi Jumatano ijayo.

Maafisa husika wa Los Angeles wamewataka watu wahame maeneo ya Encino na Brentwood ili kujikinga na moto. 

Moto uliolikumba eneo la Eaton kaskazini mwa Kaunti ya Los Angeles umeacha picha za kutisha za uharibifu. Dharura ya afya ya umma imetangazwa kwa watu wa Los Angeles sambamba na kuendelea juhudi za kupunguza hatari za kiafya kutokana na majivu na moshi unaosababishwa na moto wa porini huko Los Angeles, California.