Wataalamu wa Umoja wa Mataifa: Wanaharakati wakosoaji wa Israel sio wahalifu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122006-wataalamu_wa_umoja_wa_mataifa_wanaharakati_wakosoaji_wa_israel_sio_wahalifu
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wanaharakati wa mitandao ya kijamii wamelaani vikali kukamatwa kwa mwandishi maarufu wa habari Mmarekani mwenye asili ya Palestina katika mji wa Zurich Uswisi, wakisema kuwa kunazua wasiwasi kuhusu uhuru wa kujieleza katika nchi za Magharibi.
(last modified 2025-01-28T04:31:25+00:00 )
Jan 28, 2025 04:31 UTC
  • Wataalamu wa Umoja wa Mataifa: Wanaharakati wakosoaji wa Israel sio wahalifu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wanaharakati wa mitandao ya kijamii wamelaani vikali kukamatwa kwa mwandishi maarufu wa habari Mmarekani mwenye asili ya Palestina katika mji wa Zurich Uswisi, wakisema kuwa kunazua wasiwasi kuhusu uhuru wa kujieleza katika nchi za Magharibi.

Polisi wa Uswizi siku ya Jumamosi iliyopita walimkamata Ali Abunimah, ambaye ni mwanzilishi mwenza na mkurugenzi mtendaji wa chombo cha habari kinachounga mkono Palestina, The Electronic Intifada (EI).

Abunimah aliwasili katika uwanja wa ndege wa Zurich siku ya Ijumaa na kuhojiwa na polisi kwa saa moja kabla ya kuruhusiwa kuingia katika mji huo. Alikamatwa siku iliyofuata kabla ya kuhutubia mkutano.

Kundi la utetezi wa Wapalestina la Swiss Action for Human Rights limezindua wito wa kuachiliwa huru Abunimah.

Baada ya kukamatwa mwandishi huyo huko Uswisi, Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika maeneo yanayokaliwa, ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X akieleza wasiwasi wake juu ya hali ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari barani Ulaya.

"Mazingira yanayozunguka uhuru wa kujieleza barani Ulaya yanazidi kuwa sumu, sote tunapaswa kuwa na wasiwasi," amesema Albanese.

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa maoni na kujieleza, Irene Khan, pia amekutaja kukamatwa kwa Ali Abunimah kuwa ni "habari ya kushtua" na ameitaka Uswisi kuchunguza tukio hilo na kumwachilia huru.

Dk. Jill Stein, ambaye ni mwanafizikia na mwanaharakati wa Marekani, amesema kuwakamata waandishi wa habari hakuwezi kuzuia wimbi linaloongezeka duniani kote kupinga mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina. Jill Stein ambaye alikuwa mteule wa Chama cha Kijani kuwa mgombea wa kiti cha rais wa Merekani mnamo 2012, 2016, na 2024, amesema: Ni aibu kwa mamlaka ya Uswizi kwa kujaribu kuzuia sauti yenye nguvu ya @AliAbunimah isisikike. Upinzani dhidi ya mauaji ya kimbari ya Israel unazidi kukua barani Ulaya na duniani kote. Kuwakamata waandishi wa habari hakuwezi kukomesha wimbi hili linaloongezeka. #FreeAliAbunimah.

Craig Mokhiber, Mmarekani afisa wa zamani wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN) na mtaalamu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu, amesema kutiwa nguvuni Abunimah huko Uswisi ni jitihada za kumnyamazisha mwandishi huyo kwa niaba ya Israel na makundi yake ya mashinikizo nchini Uswizi.