Safari za Wazayuni kwenda New Zealand chini ya darubini kali
Wazayuni wanaofanya safari nchini New Zealand wapo chini ya uangalizii na darubini kali na kufanya mazingira kuwa magumu kwa wale ambao wana historia kuhudumu katika jeshi la Kizayuni.
Idara ya uhamiaji ya serikali ya New Zealand imewataka Waisraeli wanaoomba visa kutoa maelezo kama wamewahi kuhudumu katika kijeshi kama sharti la kuingia nchini humo, liliripoti gazeti la Times of Israel.
Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji ya New Zealand, Mzayuni yeyote ambaye ana historia ya kuhudumu katika jeshi la Iisrael hatopatiwa visa ya kuingia katika nchi hiyo.
Katika siku za hivi karibuni kumewasilishwa mashtaka dhidi ya wanajeshi wa Israel katika nchi mbalimbali zikiwemo Brazil, Argentina na Sri Lanka jambo ambalo limezidisha wasi wasi wa utawala wa Kizayuni kuhusu kufuatiliwa kisheria wanajeshi wa Israel kote duniani.
Vyombo vya habari vya Kiebrania vimeripoti kuhusiana na kuwasilishwa mashtaka dhidi ya mwanajeshi wa utawala wa Kizayuni huko nchini Sweden kutokana na kushiriki katika jinai za kivita huko Gaza.
Siku chache zilizopita, askari wa jeshi la Kizayuni alitoroka kutoka Brazil baada ya mahakama moja nchini humo kuamuru polisi wa nchi hiyo kumchunguza mwanajeshi wa Israel aliyesafiri hadi katika nchi hiyo akituhumiwa kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza.
Kutokana kuongezeka wasi wasi wa utawala wa Kizayuni kuhusiana na kutiwa mbaroni askari wa utawala huo katika nchi mbalimbali duniani, vyanzo vya usalama vya utawala huo vimeonya kuhusiana na suala hilo. Redio na Televisheni za Kizayuni zimeripoti kuwa, malalamiko 50 dhidi ya askari wa utawala huu yamesajiliwa katika nchi 10 za dunia.