Aliyehusika na matukio kadhaa ya kuvunjia heshima Qur'ani aangamizwa
Salwan Momika mtu aliyezua maandamano na ghasia baada ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu ameuawa kwa kupigwa risasi nchini Sweden.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari nchini humo Salwan Momika (38) anaripotiwa kuuawa katika ghorofa huko Södertälje, Stockholm, Jumatano jioni.
Polisi wa Stockholm wamesema katika taarifa kwamba watu watano wamekamatwa baada ya mtu mmoja mwenye umri wa takribani miaka 40 kupigwa risasi usiku.
Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba Momika alipigwa risasi wakati alipokuwa akizungumza mubashara kwenye mtandao wa kijamii.
Vitendo hivyo viovu vya Salwan Momika vya kuyavunjia heshima matukufu ya Uislamu viliwakasirisha Waislamu na kuwafanya waandamane mara kadhaa hadi mbele ya ubalozi wa Sweden mjini Baghdad kupinga na kulaani vitendo hivyo.
Mwaka 2023, Momika alichoma moto Msahafu mara kadhaa na kuibua hisia kali duniani za kukemewa, kupingwa na kulaaniwa kitendo chake hicho. Aliwahi kufanya kitendo hicho kiovu kwa kibali rasmi cha Polisi ya Sweden tena mbele msikiti mkuu wa Stockholm hata katika moja ya Sikukuu kubwa ya Waislamu ya Idul-Adh'ha.
Kufuatia tukio hilo, mamilioni ya Waislamu katika nchi mbalimbali walijitokeza barabarani kulaani uchomaji moto wa matukufu ya Kiislamu nchini Uswidi.
Serikali na viongozi wa Sweden ambao wamedai mara kadhaa kuwa watachunguza vitendo hivyo kisheria na kisiasa waliendelea kuunga mkono jinai hizo dhidi ya Uislamu na kuzidi kuchochea hisia za Waislamu duniani.