Kwa nini Trump anapinga sarafu moja ya BRICS?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122194-kwa_nini_trump_anapinga_sarafu_moja_ya_brics
Donald Trump amezitishia nchi wanachama wa kundi la BRICS na kuandika katika mtandao wake makhususi wa kijamii wa Truth Social kwamba atazitoza nchi hizo ushuru wa asilimia 100 ikiwa zitazindua sarafu yao ya pamoja.
(last modified 2025-02-01T23:17:44+00:00 )
Feb 01, 2025 23:17 UTC
  • Kwa nini Trump anapinga sarafu moja ya BRICS?

Donald Trump amezitishia nchi wanachama wa kundi la BRICS na kuandika katika mtandao wake makhususi wa kijamii wa Truth Social kwamba atazitoza nchi hizo ushuru wa asilimia 100 ikiwa zitazindua sarafu yao ya pamoja.

Trump ameandika: "Tutahitaji kuwajibika kwa nchi hizi zinazoonekana kuwa na uhasama kwamba zitaunda sarafu mpya ya BRICS, au kuunga mkono sarafu nyingine yoyote kuchukua nafasi ya dola ya Marekani; la sivyo zitakabiliwa na ushuru wa asilimia 100 na zitapasa kuagana na biashara katika uchumi mzuri wa Marekani." 

Hii si mara ya kwanza kwa rais mpya wa Marekani Donald Trump kutoa vitisho kwa wanachama wa BRICS kuhusu suala la kuzinduliwa sarafu ya pamoja ya nchi wanachama wa kundi hilo. Trump hata alithubutu kuzitishia nchi wanachama wa BRICS kuhusu kuzindua sarafu ya pamoja kati ya nchi hizo kabla ya kuingia White House na wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi hizo huko Russia ambapo alisema atatoza ushuru mkubwa kwa uchumi wa nchi hizo. 

Mkutano wa wakuu wa BRICS nchini Russia-2024

Swali muhimu linaloulizwa hapa ni kuwa kwa nini Donald Trump analitilia maanani sana kundi la BRICS na kujaribu kuzuia kuasisiwa sarafu moja ya kundi hilo? Sababu ya kwanza inahusiana na hali ya sasa ya sarafu ya dola duniani. Hatua ya Marekani ya kutumia sarafu ya dola kama wenzo wa kukabiliana na nchi huru imezipelekea nchi mbalimbali duniani katika kalibu ya  taasisi mbalimbali na pia katika fremu ya uhusiano wa pande mbili kutilia mkazo ulazima wa kuachana na dola katika mahusiano yao ya kiuchumi, na hivyo kuipelekea sarafu ya dola kuporomoka katika mfumo wa kimataifa. Kwa msingi huo Marekani ina wasiwasi kwamba nchi nyingi zitaacha kutumia dola kama sarafu yenye nguvu.

Gilberto Maringoni, Profesa wa Chuo Kikuu cha Sao Paulo nchini Brazil ameeleza kuwa kukataa nchi wanachama wa BRICS kutumia dola ya Marekani katika miamala na shughuli zao za kibiashara kunaweza hatimaye kusababisha kudorora Marekani. Ndio maana Rais Donald Trump wa nchi hiyo akatumia maneno ya hujuma na vitisho dhidi ya taasisi hiyo. Profesa huyu wa Brazil anasisitiza kuwa Marekani inatumia dola kueneza ukiritimba wake duniani kote. Wakati huo huo tovuti ya uchambuzi wa habari ya Bloomberg imemnukuu mwanachama wa Taasisi ya Amani ya Carnegie na kuvitaja vitisho vya Trump dhidi ya BRICS kuhusu kutumiwa sarafu nyingine ya pamoja badala ya dola kuwa ni ishara ya kuchanganyiwa serikali ya Marekani kuhusu biashara ya kimataifa.  

Profesa Gilberto Maringoni 

Sababu nyingine kubwa ni kuwa Trump ana wasiwasi kwamba mafanikio ambayo BRICS inaweza kuyapata baada ya kuunda sarafu yao moja yataibua safu ya mshikamano wa kimataifa dhidi ya matumizi ya dola; na hivyo kuiondoa dola katika biashara na shughuli mbalimbali kimataifa. Kuhusiana na hili, Tovuti ya National Interest imeripoti kuwa changamoto kubwa inayoikabili Washington si tu kuhusiana na kupoteza udhibiti wake kwa sarafu ya dola, bali ni safu mpya ya mshikamano wa kimataifa unaoshuhudiwa sasa ambao unapunguza ushawishi wake duniani. 

Sababu ya tatu yenye umuhimu kuhusu vitisho vya Trump dhidi ya BRICS ni kuhusu nafasi ya kimataifa ya kundi hili pamoja na nguvu na uwezo wa wanachama wake. Kundi la BRICS, ambalo wanachama wake ni pamoja na madola makubwa ya dunia na baadhi ya nchi za kikanda kama China, Russia, India, Iran, Brazil na Afrika Kusini limekuwa jukwaa la kimataifa la kushughulikia migogoro mikubwa, kubadilisha mfumo wa biashara ya kimataifa, na kusaidia miradi mbalimbali. Nchi za BRICS zinaunda asilimia 42 ya watu wote duniani, asilimia 30 ya ardhi ya dunia na kudhamini asilimia 24 ya uchumi wa dunia. Nchi kubwa kama China ambayo ni mshindani muhimu zaidi wa kiuchumi wa Marekani duniani ni miongoni mwa wanachama waanzilishi wa BRICS; na Trump pia amejikita kukabiliana na nafasi na ushawishi unaoimarika wa Beijing kimataifa. Ndio maana rais huyo mpya wa Marekani akaitishia pia BRICS na kupinga vikali sarafu ya pamoja ya taasisi hiyo. 

BRICS dhidi ya matumizi ya dola