Kundi la Hague ni nini na kwa nini limeanzishwa?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122232-kundi_la_hague_ni_nini_na_kwa_nini_limeanzishwa
Baada ya kutangazwa usitishaji mapigano na kupita miezi 15 ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, nchi tisa kutoka Asia, Afrika na Amerika ya Kusini zimeunda kundi lililopewa jina la The Hague Group kwa ajili ya kutetea Palestina.
(last modified 2025-02-02T09:04:27+00:00 )
Feb 02, 2025 09:04 UTC
  • Kundi la Hague ni nini na kwa nini limeanzishwa?

Baada ya kutangazwa usitishaji mapigano na kupita miezi 15 ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, nchi tisa kutoka Asia, Afrika na Amerika ya Kusini zimeunda kundi lililopewa jina la The Hague Group kwa ajili ya kutetea Palestina.

Katika mkutano uliofanyika The Hague huko Uholanzi, ulioandaliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa, wawakilishi wa nchi hizo tisa wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kidiplomasia na kiuchumi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa huko Gaza.

Baada ya mazungumzo hayo, wawakilishi kutoka Afrika Kusini, Malaysia, Namibia, Colombia, Bolivia, Chile, Senegal, Honduras na Belize wametangaza kwamba wameunda kundi hilo ili kutetea haki za Wapalestina. Taarifa iliyotolewa na nchi hizo tisa inasema: "Hatuwezi kuwa kimya mbele ya jinai za kimataifa na tumeazimia kutimiza ahadi zetu za kukomesha uvamizi wa Israel katika nchi ya Palestina na kusaidia juhudi za kupatikana haki ya watu wa Palestina ya kujitawala, ikiwa ni pamoja na haki ya kuwa na taifa huru la Palestina."

Wawakilishi wa nchi za The Hague Group

Mojawapo ya matokeo ya miezi 15 ya jinai na mauaji ya kimbari ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza ni kufichuliwa sura halisi ya utawala bandia na unaouawa watoto wa Israel ambao misingi yake imewekwa juu ya sera ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za nchi nyingine, kuua raia na kuwafukuza mamilioni ya Wapalestina kwenye makazi yao. Katika kipindi chote cha miaka 76 kuwepo kwake, Israel haijawahi kupingwa katika majukwaa ya kimataifa kwa kiasi hiki cha sasa. Katika kipindi cha miongo saba iliyopita, Wazayuni daima wamejaribu kuhalalisha uvamizi na kuzikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina kwa simulizi za uongo kuhusu kuwepo Mayahudi huko Palestina. Katika mkondo huo, upinzani na ukosoaji wa aina yoyote wa walimwengu hususan katika nchi za Magharibi dhidi ya sera hizo za kikoloni umetajwa kuwa ni chuki dhidi ya Uyahudi. Ukosoaji na maandamano dhidi ya jinai za Israel unamfanya mhusika aadhibiwe kwa kufukuzwa kazi, kutozwa faini na kifungo jela. Hata hivyo, katika kipindi cha miezi 15 iliyopita, walimwengu wamekuwa na mwamko mkubwa kuhusu hali ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Hivi karibuni, Kituo cha habari, The Palestinian European Media Center, kilitangaza kuwa Ulaya imeshuhudia maandamano na mijumuiko zaidi ya 30,000 katika miji 619 na nchi 20 katika siku 470 za vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Maandamano dhidi ya Israel katika nchi za Magharibi

Suala jingine lililosababishwa na mwamko wa fikra za umma wa walimwengu hususan katika nchi za Magharibi kuhusiana na Israel ni harakati za baadhi ya taasisi za kimataifa dhidi ya Wazayuni licha ya ushawishi mkubwa wa nchi za Ulaya na Marekani katika taasisi hizo. Baadhi ya nchi kama Afrika Kusini, ambayo ni miongoni mwa wahanga wa ubaguzi wa rangi, zimejaribu kutumia uwezo wote wa taasisi za kimataifa kulaani jinai za Wazayuni na kusimamisha mauaji ya Israel huko Gaza. Mnamo Disemba 2023, Afrika Kusini iliituhumu Israel kuwa imefanya mauaji ya kimbari huko Gaza, ikitumia Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari (1948). Kesi hiyo, iliyoimarishwa na kupata nguvu zaidi baada ya kujiunga nchi kama Colombia, Nicaragua na Mexico katika mashtaka hayo, inasisitiza "haja ya dharura ya kukomeshwa ukatili wa Israel." Mnamo Januari 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilitoa amri za muda zilizoitaka Israel kusitisha vitendo vya mauaji ya kimbari na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafika kwa watu wa Gaza. Japokuwa Wazayuni na waungaji mkono wao, yaani Marekani na Ulaya, hawakutekeleza hukumu hiyo, lakini kutolewa kwake pekee lilikuwa pigo la kisheria na kisiasa kwa sura ya utawala bandia wa Israel katika uga wa kimataifa.

Kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Afrika Kusini, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) pia, ilimpata Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa vita wa utawala huo, Yoav Gallant na hatia ya kufanya uhalifu wa kivita na kutoa hati ya kukamatwa kwao katika kila nchi mwanachama wa mahakama hiyo.

Israel imeua maelfu ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, wengi ni wanawake na watoto.

Hivi sasa, hatua zimechukuliwa na baadhi ya nchi kwa ajili ya kukomesha vita vya utawala unaoua watoto wa Israel katika uwanja wa kimataifa. Awali, lilikuwa jambo lisilofikirika kuwa nchi hizo ambazo hazikuwa na ushawishi katika ulingo wa kimataifa zingeweza kutoa changamoto si kwa utawala bandia wa Israel pekee bali pia kwa serikali za nchi za Ulaya na Marekani zinazounga mkono jinai za Israel kwa hali na mali. Aghalabu ya nchi za Ulaya zinazouunga mkono utawala bandia wa Israel ni wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na sasa ziko katika hali ambayo, kinyume na matakwa yao, zinalazimika ziwatie nguvuni Netanyahu na Gallant iwapo watasafiri kwenda Ulaya.

Wazayuni hawakushindwa na wapiganaji wa Hamas na Palestina katika vita huko Gaza pekee, bali kuundwa Kundi la Hague (The Hague Group) lililoanzishwa na nchi za Asia, Afrika na Amerika ya Kusini kwa ajili ya kuitetea Palestina, kunaonyesha kuwa, mapambano dhidi ya Wazayuni yanaendelea katika medani ya kimataifa.