Vipi Canada na Mexico zimeingia katika vita vya kibiashara na Marekani?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122280-vipi_canada_na_mexico_zimeingia_katika_vita_vya_kibiashara_na_marekani
Baada ya Rais Donald Trump kuanzisha vita vya kibiashara dhidi ya Canada na Mexico kwa kuweka ushuru wa 25% kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka katika nchi hizo, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau ametangaza ushuru wa 25% kwa bidhaa zilizoagizwa kutoka Merika kama hatua ya kulipiza kisasi.
(last modified 2025-02-03T22:54:23+00:00 )
Feb 03, 2025 22:54 UTC
  • Vipi Canada na Mexico zimeingia katika vita vya kibiashara na Marekani?

Baada ya Rais Donald Trump kuanzisha vita vya kibiashara dhidi ya Canada na Mexico kwa kuweka ushuru wa 25% kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka katika nchi hizo, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau ametangaza ushuru wa 25% kwa bidhaa zilizoagizwa kutoka Merika kama hatua ya kulipiza kisasi.

Siku ya Jumamosi, Trump alitangaza ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Canada, China, na Mexico, washirika watatu wakubwa wa kibiashara wa Marekani. Mexico na Canada zimeapa kulipiza kisasi kwa hatua hiyo ya Trump, wakati China ikisema itapinga hatua hiyo katika Shirika la Biashara Duniani na kuchukua "hatua zingine" za kujibu mapigo.

Saa chache baada ya hatua hiyo ya Trump, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau ametangaza ushuru wa 25% kwa bidhaa za Marekani ambazo "zitajumuisha bidhaa za kila siku kama hatua ya, kulipiza kisasi." Trudeau amesema, "Hatua ya Trump haitawadhuru Wacanada pekee, bali itakuwa na "matokeo hasi" kwa wananchi wa Marekani."

Kadhalika Rais Claudia Sheinbaum wa Mexico pia alitangaza siku ya Jumamosi kuwa, Mexico italipiza kisasi dhidi ya ushuru mpya uliowekwa na Trump kwa ushuru zaidi kwa bidhaa za Marekani, na hatua zingine zitakazoamuliwa baadaye.

Rais wa Marekani pia alitangaza kutoza ushuru wa 10% kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini China na kutangaza kuwa katika wiki zijazo, ongezeko la ushuru pia litatumika kwa bidhaa za Ulaya.

Trump ametangaza ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Canada, China, na Mexico.

 

Beijing iliitangaza jana Jumapili kuwa "inapinga vikali" ushuru uliowekwa na US dhidi ya Beijing, na kusisitiza kuwa itachukua "hatua zinazolingana ili kulinda kwa uthabiti haki na masilahi ya China."

Liu Pengyu, msemaji wa ubalozi wa China mjini Washington, alisema baada ya kutekelezwa kwa ushuru huo mpya: "Ikiwa kuna tofauti na msuguano kati ya pande hizo mbili, zinapaswa kutatuliwa kwa mazungumzo na mashauriano." Hakuna mshindi katika vita vya kibiashara au vita vya ushuru vinavyonufaisha upande mmoja au dunia.

Ijapokuwa Donald Trump alizungumza tangu mwanzo wa kinyang'anyiro cha urais kuhusu kutoza ushuru mkubwa wa forodha kushughulikia uagizaji wa bidhaa za kigeni na kuimarisha sekta ya viwanda nchini Marekani, lakini weledi wengi wa mambo wanaona kuwa, utekelezaji wa sera hiyo sio hatua sahihi na hilo litakuwa sababu ya kuongezeka kwa mvutano na mfumuko wa bei ndani na nje ya Marekani. Hata hivyo, Trump amepuuza mtazamo huo na ametoa agizo la kutekelezwa mpango huo.

Trump daima amezingatia biashara huria kuwa sababu kuu ya kuyumba uchumi wa Marekani, kwa hivyo anazingatia kutozwa ushuru mkubwa kuwa ni kikwazo kwa tatizo hili. Hii ni katika hali ambayo, kwa mtazamo wa viongozi wa mataifa mengi makubwa duniani hususan nchi zinazoibukia kiuchumi na nchi zinazoelekeza mauzo ya nje ni kwamba, kupitishwa kwa sera za kupinga uhuru wa biashara, sio tu kwamba itakuwa na athari mbaya kwa uchumi wa dunia, lakini pia itakuwa na athari mbaya kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi zinazotekeleza sera hiyo. Katika suala hili, hata Trump mwenyewe anakiri kuhusiana na matokeo hasi ya vita vya ushuru kwa maisha ya watu wa Marekani, lakini anaamini kuwa athari hizo mbaya ni za muda mfupi.

 

Ingawa Rais mpya wa Marekani ana nia ya kuimarisha uchumi wa ndani wa Marekani na kuwahimiza raia wa nchi hiyo kununua bidhaa za Marekani kwa kuingia katika vita vya biashara, lakini inaonekana kuwa, katika muda mrefu sera hii haitaathiri Marekani na washirika wake tu wa kibiashara, lakini pia uchumi wa dunia, kwa sababu utekelezaji wa sera hiyo katika muda mrefu, unatishia ukuaji wa biashara ya kimataifa pamoja na misingi ya mfumo wa biashara wa pande kadhaa na wenye nidhamu.

Pia, miongoni mwa madhara ya utekelezaji wa sera hiyo, kuna kuyumba kwa soko la biashara na malighafi duniani, kukua kwa madeni ya nje na kukosekana kwa usawa katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande mwingine, matokeo ya sera hizo yanaweza pia kusababisha kutengwa Marekani kwa sababu hata washirika wengi wa Marekani wamefikia natija hii kwamba Washington sio mshirika wa kibiashara na kisiasa wa kuaminika, kwa hivyo, katika muda mrefu, wataimarisha ushirikiano wa kikanda na baina ya nchi mbili bila ya kuishirikisha Washington.

Kuundwa makundi na jumuiya kama vile BRICS pamoja na miungano ya kikanda ni hatua ambazo zimekaribishwa kwa mikono miwili na mataifa ya dunia, suala ambalo Trump hawezi kulistahimili.

Filihali nchi kama Canada, Mexico na China zimetangaza kupinga hatua hiyo ya Trump, na inaonekana Trump ameanza kucheza kamari ngumu kabisa ya kiuchumi.