Walimwengu waendelea kukataa mpango wa Trump wa kuitwaa Gaza
Mpango wa Trump wa kuitwaa Gaza umeendelea kupingwa kkatika kila kona ya dunia.
Rais wa Palestina amekataa vikali pendekezo la Rais Donald Trump la Marekani kuitwaa Gaza na kuwahamisha wakazi wa Wapalestina milioni 2.1 wanaoishi huko.
"Hatutaruhusu haki za watu wetu, kukiukwa," amesema Mahmoud Abbas, akionya kwamba Gaza ni "sehemu muhimu ya Palestina" na kuwahamisha watu kwa nguvu utakuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Gaza ni sehemu muhimu ya taifa la baadaye la Palestina. Amesema huko New York kwamba haki za Wapalestina kuishi kama binadamu katika ardhi yao zinazidi kukiukwa.
Ismail Baqaei msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepinga vikali mpango wa Marekani wa kutaka kuinyakua na kuitwaa Gaza, na kusema kutolewa fikra kama hiyo ni jambo la kushangaza linalokwenda sambamba na mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuiangamiza kabisa Palestina.
Saudi Arabia imesema Wapalestina "hawatahama" kutoka katika ardhi yao.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesisitiza kuwa msimamo wa nchi hiyo kuhusu suala la kuundwa nchi huru ya Palestina ni thabiti, wa kimsingi na hauwezi kubadilika.
Aidha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), imepinga mpango huo wa Donald Trump na kueleza kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Radiamali hizo zinatolewa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza hadharani kwamba Marekani itatwaa na kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjini Washington.