Cuba: Kuna ulazima wa nchi huru ya Palestina kutambuliwa rasmi
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba ametangaza kuwa taifa huru la Palestina linapaswa kutambuliwa na mjim Baytul-Muqaddas Mashariki ukiwa mji mkuu wake.
Bruno Eduardo Rodríguez, amesema hayo katika kujibu pendekezo la Rais wa Marekani kuhusu kulazimishwa kuhama Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amesisitiza kuwa, Gaza ni mali ya watu wa Palestina na kwamba, Israel na muungaji mkono wake yaani Marekani wanapaswa kudiriki na kuheshimu hilo.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amebainisha kwamba, njia pekee inayowezekana ya kumaliza mzozo wa sasa ni kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina kwenye mipaka ya kabla ya 1967 na Quds Mashariki ukiwa mji mkuu wake.
Hayo yanajiri katikka hali ambayuo, hivi majuzi Rais wa Cuba alisema kuwa, muqawama wa taifa la Palestina ni mapambano bora zaidi duniani.
Rais Miguel Diaz-Canel sambamba na kuashiria kwamba maadui wataendelea na njama zao za kuliangamiza suala la Palestina amesema: "Muqawama wa watu wa Palestina ni mfano bora zaidi wa mapambano na kusimama kidete katika dunia ya leo.
Viongozi wa Cuba wamekuwa wakiukosoa mara kwa mara ukatili wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na pia wametaka kumalizika kwa vita vya Gaza na kusitishwa mauaji ya raia wa Gaza. Hivi karibuni, serikali ya Cuba ilitangaza kuwa, kama sehemu ya dhamira yake ya dhati ya kusaidia juhudi halali za kimataifa za kumaliza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina, imejiunga na kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.