Rais wa Marekani anataka kunyakua Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122438-rais_wa_marekani_anataka_kunyakua_ukanda_wa_gaza
Katika taarifa isiyo na mfano wake na ya ghafla, Rais wa Marekani amesema mbele ya Waziri Mkuu wa Israel huko White House kwamba Marekani inanuia kuutwaa Ukanda wa Gaza na pia kuwa kuna uwezekano wa nchi hiyo kutambua rasmi udhibiti wa utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2025-02-07T08:40:25+00:00 )
Feb 07, 2025 08:40 UTC
  • Rais wa Marekani anataka kunyakua Ukanda wa Gaza

Katika taarifa isiyo na mfano wake na ya ghafla, Rais wa Marekani amesema mbele ya Waziri Mkuu wa Israel huko White House kwamba Marekani inanuia kuutwaa Ukanda wa Gaza na pia kuwa kuna uwezekano wa nchi hiyo kutambua rasmi udhibiti wa utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Msimamo huu mpya wa serikali ya Marekani unaashiria kuwa Trump anataka kugawana ardhi iliyosalia ya Wapalestina baina yake na Wazayuni kwa ushirikiano wa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel. Bila shaka, katika kuhalalisha mpango wake wa kunyakua Ukanda wa Gaza, Trump ameashiria uharibifu wa kutisha na wa kushtua uliofanywa katika ardhi hiyo na Wazayuni wakati wa vita vya miezi 15. Amesema: "Ukanda wa Gaza si mahali pazuri kwa Wapalestina kuishi na wanapaswa kupatiwa kipande kingine cha ardhi kizuri na kipya."

Awali, Trump alisema kuwa Wapalestina wanaoishi Gaza wanapaswa kuhamishiwa Misri na Jordan ili Gaza iweze kujengwa upya. Sasa rais ameenda mbali zaidi na kuzungumzia unyakuzi wa kipande hiki kidogo cha ardhi lakini chenye watu wengi zaidi duniani kilichoko kwenye ufuo wa mashariki wa Bahari ya Mediterania. Mtu huyu ambaye alifanya kazi katika tasnia ya ujenzi alipokuwa na umri mdogo na sasa ni rais wa Marekani, anapanga njama ya kuwafukuza wakazi wa eneo hilo lililoharibiwa na vita, kwa kutumia visingizio vya kibinadamu. Hii ni pamoja na kuwa hana nia yoyote ya kuuliza wala kujua maoni ya wakazi hao kuhusu suala hilo. Hii ndio maana anazungumza bila kujali kuhusu ulazima wa kutimuliwa watu milioni mbili na nusu wanaoishi Gaza. Kuhusu zaidi ya Wapalestina milioni tatu wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi pia, amesema kuna uwezekano wa kutwaliwa na kuunganishwa ardhi yao na ile inayokaliwa kwa mabavu na Israel tangu 1948. Kwa njia hii, wazo la suluhisho la serikali mbili kati ya Wazayuni na Wapalestina litatupiliwa mbali na serikali ya sasa ya Marekani, na hivyo kuandaa uwanja wa ardhi zilizosalia za Wapalestina kutwaliwa na Israel.

Trump (kushoto) akiwa na Netanyahu, mshirika wake wa karibu katika mauaji ya Wapalestina

 

Ni wazi kuwa kufikia sasa, nchi zote za Kiarabu zimepinga kwa kauli moja mpango huo wa Trump wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza na kuwapeleka Misri na Jordan. Hata hivyo, Trump anajulikana kwa kutumia ushawishi wa kisiasa na kiuchumi pamoja na nguvu za vitisho za jeshi la Marekani dhidi ya nchi za Kiarabu, hasa Misri na Jordan. Kwa maneno mengine ni kuwa ikiwa jeshi la Marekani litatumwa katika eneo kudhibiti Gaza na kufungua mipaka ya Misri kwa nguvu ili mamia ya maelfu ya Wapalestina wasukumwe ndani ya ardhi ya Misri, Cairo haitakuwa na ujasiri wa kupinga hatua hiyo.

Pamoja na hayo ni jambo lisilowezekana kwamba Wapalestina, taifa ambalo halijaacha kupigania ukombozi wa ardhi yao licha ya siasa za uvamizi, vita na mauaji ya umati kwa miaka 80 iliyopita, watakaa kimya na kujisalimisha mbele ya uvamizi wa Marekani. Kwa maelezo hayo, ni wazi kuwa kinyume na madai ya Trump ya eti kuleta amani katika eneo la Asia Magharibi na kuwaandalia mamialioni ya Wapalestina maisha ya amani, rais huyo mpya wa Marekani kwa hakika anawasha moto wa vita vipya katika eneo, moto ambao si tu kwamba utaziteketeza nchi za eneo, bali pia utawakumba Wamarekani kama sehemu ya majeshi yanayoikalia kwa mabavu Palestina.

Amani na utulivu utarejea katika ardhi ya Palestina pale tu dhulma dhidi ya mamilioni ya Wapalestina itakapoondolewa na waruhusiwe kujiundia nchi wanayoitaka. Vinginevyo, kukaliwa kwa mabavu Gaza na Wamarekani au kutambuliwa rasmi mamlaka ya Israel juu ya Ukingo wa Magharibi litakuwa tu ni jaribio la kufunika tatizo hilo sugu bila kutafutiwa suluhu ya kudumu.