Uswisi yamchunguza mwanajeshi wa Israel anayetuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122448-uswisi_yamchunguza_mwanajeshi_wa_israel_anayetuhumiwa_kufanya_uhalifu_wa_kivita_gaza
Uswisi imeanza kufanya uchunguzi wa jinai dhidi ya mwanajeshi Mzayuni anayeishi nchini humo kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita wakati wa vita vya utawala wa Israel dhidi ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-02-07T22:59:12+00:00 )
Feb 07, 2025 22:59 UTC
  • Uswisi yamchunguza mwanajeshi wa Israel anayetuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita Gaza

Uswisi imeanza kufanya uchunguzi wa jinai dhidi ya mwanajeshi Mzayuni anayeishi nchini humo kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita wakati wa vita vya utawala wa Israel dhidi ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza.

Ripoti zinasema, Uswisi imeanzisha uchunguzi dhidi ya mwanajeshi wa utawala wa Israel anayeshukiwa kufanya uhalifu wa kivita katika katika Ukanda wa Gaza.

Mashtaka dhidi ya mwanajeshi huyo wa utawala wa Kizayuni yana ushahidi mwingi unaoonyesha kuwa alishiriki katika jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza.

Katika siku za hivi karibuni kumewasilishwa mashtaka dhidi ya wanajeshi wa Israel katika nchi mbalimbali zikiwemo Brazil, Argentina na Sri Lanka jambo ambalo limezidisha wasi wasi wa utawala wa Kizayuni kuhusu kufuatiliwa kisheria wanajeshi wa Israel kote duniani.

Majuma machache yaliyopita, askari wa jeshi la Kizayuni alitoroka kutoka Brazil baada ya mahakama moja nchini humo kuamuru polisi wa nchi hiyo kumchunguza mwanajeshi wa Israel aliyesafiri hadi katika nchi hiyo akituhumiwa kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza.

Wakati huo huo, idara ya uhamiaji ya serikali ya New Zealand imewataka Waisraeli wanaoomba visa kutoa maelezo kama wamewahi kuhudumu katika kijeshi kama sharti la kuingia nchini humo. Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji ya New Zealand, Mzayuni yeyote ambaye ana historia ya kuhudumu katika jeshi la Iisrael hatopatiwa visa ya kuingia katika nchi hiyo.

Kutokana kuongezeka wasi wasi wa utawala wa Kizayuni kuhusiana na kutiwa mbaroni askari wa utawala huo katika nchi mbalimbali duniani, vyanzo vya usalama vya utawala huo vimeonya kuhusiana na suala hilo. Redio na Televisheni za Kizayuni zimeripoti kuwa, malalamiko 50 dhidi ya askari wa utawala huu yamesajiliwa katika nchi 10 za dunia.