Independent: Chuki dhidi ya Waislamu nchini India zimeongezeka mnamo 2024
Ripoti iliyochapishwa na The Independent imefichua ongezeko kubwa la matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu wa India na dini nyingine za waliowachache, na kumeripotiwa ongezeko la 75% katika 2024 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.
Ripoti hiyo iliyotegemea utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Chuki Iliyopangwa mjini Washington, ilibaini kuwa India ilishuhudia matukio 1,165 yanayohusiana na matamshi ya chuki, 98.5% yakiwalenga Waislamu, huku takriban 10% yakiwa ni mashambulizi dhidi ya Wakristo.
Utafiti wa kituo hicho umemulika zaidi ongezeko la kutisha la matamshi ya chuki katika majimbo yanayotawaliwa na Chama cha Bharatiya Janata, na karibu 80% ya matukio (931) yakitokea katika majimbo hayo.
Kinyume chake, 2% tu ya matukio (234) ya hujuma na matukio ya chuki dhidi ya Waislamu yalitokea katika majimbo yanayotawaliwa na upinzani, jambo ambalo inathibitisha -kwa mujibu wa ripoti hiyo- kuwepo uhusiano mkubwa kati ya utawala wa Waziri Mkuu, Narendra Modi, na kuenea kwa matamshi ya chuki.
Majimbo ya Uttar Pradesh, Maharashtra na Madhya Pradesh yamechangia karibu nusu ya matukio hayo, huku matukio ya matamshi ya chuki yakishika kasi wakati wa uchaguzi mkuu wa 2024.
Ripoti hiyo imesema kuwa matamshi ya chuki yamebadilika kutoka kuwa chombo cha kisiasa cha kuzusha migawanyiko wa kidini na kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa kisiasa wa India na kampeni za uchaguzi.