Mahakama ya ICC: Tunalaani vikwazo vya Marekani kwa mwendesha mashtaka wetu
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyoko The Hague huko Uholanzi imetoa taarifa ikilaani hatua ya utawala wa Donald Trump kumuwekea vikwazo Mwendesha Mashtaka wa mahakama hiyo, Karim Khan.
Taarifa ya ICC imesisitiza kuwa: "Tunajitolea kuendelea na majukumu yetu ya kisheria kwa maslahi ya mamilioni ya waathiriwa wasio na hatia wa uhalifu."
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imeongeza kuwa: "Tunatoa wito kwa nchi zote za dunia na mashirika ya kiraia kuungana ili kuhakikisha haki inatekelezwa katika ngazi ya kimataifa."
Alkhamisi iliyopita, Trump alitoa amri ya kiutendaji ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), iliyoko Uholanzi, akiunga mkono na kuukingia kifua utawala wa Kizayuni wa Israel, wakati Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu akiwa Washington, DC. Netamyahu na aliyekuwa waziri wake wa vita, Yoav Gallant wanasakwa na mahakama hiyo kujibu tuhuma za kufanya mauaji ya kimbari, kutenda jinai za kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Ijumaa iiliyopita pia Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz alikosoa uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Junai akiitaja kuwa ni hatua isiyo sahihi.
Scholz alikiri kwamba vikwazo hivyo vinahatarisha utendakazi wa taasisi ambayo inapaswa kuhakikisha kuwa madikteta kote duniani hawawezi kuwanyanyasa watu na kuanzisha vita.
Televishenii ya NBC pia imeripoti kuwa nchi 79 zikiwemo Canada, Ujerumani, Ufaransa, Afrika Kusini na Mexico zimetangaza katika taarifa yao ya pamoja kwamba hatua ya Trump ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu inaharibu utawala wa sheria wa kimataifa.