Hatua za awali za kumaliza vita ya Ukraine na mustakabali usiojulikana
Baada ya Russia kumuachilia mfungwa Mmarekani, kitendo ambacho Rais wa Marekani alikielezea kama juhudi ya kumaliza vita vya Ukraine, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alitangaza kwamba yuko tayari kubadilishana ardhi na Russia.
Russia ilimwachilia Marc Hilliard Fogel, mfungwa Mmarekani, baada ya ziara ya ghafla ya mjumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff kwenda Moscow. Kufuatia kuachiliwa kwa Fogel, Donald Trump alielezea uamuzi wa Russia kama hatua ya kuelekea kumaliza vita vya Ukraine na kusema: "Russia ilitutendea vizuri sana. Kwa kweli, ninatumai hii ni mwanzo wa uhusiano ambao tunaweza kumaliza vita."
Katika muktadha huu, Rais Zelensky wa Ukraine pia ameonyesha mabadiliko makubwa katika msimamo wake na kusema kwamba nchi yake itakubali kubadilishana eneo la ardhi na Russia. Aliongeza kuwa nchi yake haiwezi kupata dhamana za usalama pekee kutoka kwa washirika wa Ulaya, na kwamba dhamana ya usalama bila Marekani haiwezi kuwa ya kweli. Kauli za Zelensky zilitolewa wakati ambapo awali, Rais wa Ukraine alikuwa akisisitiza kutokubali kuachia hata chembe ya ardhi yoyote kwa Urusi.
Pamoja na mabadiliko haya, bado hakuna mtazamo wazi wa kumaliza vita vya Ukraine. Rais Donald Trump wa Marekani aliahidi kumaliza vita vya Ukraine kwa haraka katika kampeni yake ya uchaguzi, lakini inaonekana kuwa viongozi wa Washington bado hawana mpango mzuri na wa kujadiliana kuhusu jinsi ya kumaliza vita. Kwa upande huu, gazeti la Times lilielezea hivi: "Mustakabali wa Ukraine katika vita na Russia haujawahi kuwa mweusi zaidi kuliko sasa. Ukraine bado haijasambaratika lakini kwa hakika imepata kipigo kikubwana imepigishwa magoti."
Katika uwanja wa vita, Ukraine imekuwa ikirudi nyuma katika miezi ya hivi karibuni. Ripoti zinaonyesha kuwa wanajeshi wa Russia walifaulu kuchukua udhibiti wa maeneo zaidi ya Ukraine mara sita zaidi mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka 2023. Kwa tathmini zilizofanywa, Ukraine imepoteza zaidi ya 20% ya ardhi yake. Jarida la Economist* liliripoti kuhusu hili na kusema: "Viongozi wa Ukraine wanakabiliwa na uhaba wa wanajeshi wa kujitolea na hali itakuwa mbaya zaidi, kwani wengi wa wanajeshi hawa wanataka kuachia maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Russia kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo na kurejea amani; katika muktadha huu, mmoja wa makamanda wa uwanja wa vita wa jeshi la Ukraine alisema: 'Asilimia 70 ya jeshi linaafiki kutopigana kukomboa ardhi zilizochukuliwa na Russia."
Kwa upande mwingine, hali ya Ulaya na Ukraine imekuwa ngumu zaidi tangu kuanza kwa utawala wa Trump. Nchi za Ulaya sasa hazina uwezo wa kutuma msaada wa kifedha na kijeshi kwa Ukraine kama ilivyokuwa awali, na kwa upande mwingine, msaada kutoka Washington kwa Ukraine pia uko katika hali ya kutatanisha.
Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa zamani wa NATO ambaye amemaliza majukumu yake hivi karibuni, alisema: "Tunahitaji mpaka kwa ajili ya kusimamisha mapigano na bila shaka mpaka huu katika hali bora unapaswa kujumuisha maeneo yote ambayo Russia inadhibiti sasa."
Hali hii inajiri wakati ambapo Rais Vladimir Putin wa Russia amekariri mara kadhaa masharti yake kwa ajili ya kumaliza vita vya Ukraine, ikiwa ni pamoja na kutojiunga kwa Ukraine na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Atlantiki ya Kaskazini (NATO), kuondolewa kwa vikwazo vyote vya Magharibi dhidi ya Russia na uondoaji kamili wa wanajeshi wa Ukraine kutoka maeneo ya Donbas na Novorossiya.
Ingawa sasa, tangazo la Ukraine la kuwa tayari kubadilishana ardhi na Russia linaweza kuchukuliwa kama ishara ya utayari wa nchi hii kuanzisha mazungumzo ya amani na juhudi za kumaliza vita, bado kuna changamoto nyingi katika njia hii, ambapo sharti la Russia la Ukraine kutojiunga na NATO ni moja ya masuala muhimu zaidi.