Iran yapania kuimarisha uhusiano na nchi za bara Asia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12274-iran_yapania_kuimarisha_uhusiano_na_nchi_za_bara_asia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha uhusiano wake na nchi za bara Asia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 30, 2016 08:17 UTC
  • Iran yapania kuimarisha uhusiano na nchi za bara Asia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha uhusiano wake na nchi za bara Asia.

Hayo yamesemwa na Ebrahim Rahimpour, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika mazungumzo yake na Retno Marsudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia mjini Jakarta hapo jana na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN katika nyuga tofauti.

Retno Marsudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia

Rahimpour amesema Indonesia ni nchi muhimu katika sera za mambo ya nje ya Iran na kwamba, safari inayotazamiwa karibuni hivi ya Rais Joko Widodo wa Indonesia mjini Tehran itakuwa na nafasi muhimu katika kuharakisha utekelezwaji wa makubaliano kati ya nchi mbili hizo.

Kadhalika Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza juu ya umuhimu wa Tehran na Jakarta kuimarisha uhisiano wao wa kibenki kwa shabaha ya kuboresha biashara kati ya nchi mbili hizo.

Kwa upande wake, Retno Marsudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia amesema Jakarta inaihesabu Iran kuwa rafiki wake wa karibu na kwamba iko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika kiwango cha kieneo na kimataifa.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN ni pamoja na Indonesia, Malaysia, Ufilipino, Singapore na Thailand huku nchi za hivi karibuni kujiunga na jumuiya hiyo iliyobuniwa mwaka 1967 zikiwa ni Brunei, Cambodia, Laos, Myanmar na Vietnam.