Marufuku ya TikTok nchini Marekani inalenga kukandamiza maudhui dhidi ya Israel
Marufuku ya TikTok nchini Marekani ilichochewa na Israel na inalenga kukandamiza wenye kusambaza maudhui zinazounga mkono Palestina na kulaani Israel.
Hatua hiyo imekuja baada ya vijana wengi wa Marekani kupinga vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza.
Kwa mujibu wa taarifa, Kongresi ya Marekani imepitisha marufuku ya TikTok, inayomilikiwa na China, kwa kisingizio cha usalama wa taifa.
Mtandao huo wa kijamii ulizimwa nchini Marekani mwezi uliopita, kabla ya kuidhinishwa tena hewani wiki hii baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahirisha marufuku hiyo.
Mwandishi wa habari wa Marekani Ken Klippenstein alisema Jumapili kuwa “Kumilikiwa TikTok na kampuni ya China haikuwa sababu kuu iliyosababisha Kongresi kuchukua hatua.”
Alibainisha kuwa muswada wa usalama wa taifa “ulikuwa umekufa” hadi operesheni ya Hamas ya Oktoba 7, 2023, iitwayo Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya Israel, “iliyorejesha sheria hiyo kuwa hai tena.”
Seneta Mitt Romney, anayeunga mkono marufuku ya TikTok, alihusisha uungaji mkono wake wa kuzima jukwaa hilo maarufu miongoni mwa vijana wa Marekani na suala la Palestina.
Maandamano ya kuunga mkono Palestina yalianza katika Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York mnamo Aprili 17, 2024, kisha yakaenea katika vyuo vingine kote Marekani, yakiunda vuguvugu la wanafunzi lisilokuwa na mfano wake katika karne hii.
Waandamanaji, walitaka kukomeshwa kwa vita vinavyoungwa mkono na Marekani, ambavyo vimesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 48,271, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine 111,693. Aghalabu ya vijana hao ambao walikabiliwa na ukatili wa polisi, wamekuwa wakitumia jukwaa la TikTok kuhamasishana kuhusu kadhia ya Palestina.