Je, BRICS inafuatilia sera zipi katika duru hii mpya?
Brazil, ikiwa mwenyekiti mpya wa kundi la BRICS, imefafanua mipango ya kundi hili katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, kisiasa na kiusalama.
Brazil, ambayo hivi karibuni imechukua uenyekiti wa kundi la BRICS, imetangaza kwamba kundi hilo litapanua shughuli zake katika maeneo sita ambayo ni biashara na fedha, afya ya kimataifa, mabadiliko ya hali ya hewa, amani na usalama wa kimataifa, udhibiti wa Akili Mnemba na kurekebisha muundo wa amani na usalama duniani.
Kundi la BRICS, ambalo limekuwa moja ya makundi yenye ushawishi mkubwa katika uchumi na siasa za dunia katika miaka ya hivi karibuni, linajumuisha nchi za Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Misri, Indonesia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Indonesia, ambapo nchi nyingine kadhaa pia zinashiriki katika vikao vya kundi hilo kama washirika wa BRICS. Brazil imechukua uenyekiti wa zamu wa BRICS katika kipindi hiki cha 2025.
Katika miaka ya hivi karibuni, wanachama wa BRICS wamejaribu kuboresha hali ya kiuchumi ya nchi wanachama na kuimarisha ushirikiano wa kieneo kwa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na kimataifa katika sekta za biashara na fedha.
Kuhusiana na hili, kuondolewa dola katika miamala ya kibiashara na kifedha na wakati huo huo kukabiliana na satwa ya Marekani kunachukuliwa kuwa mojawapo ya malengo muhimu zaidi ya kundi hili, ambapo imekubaliwa kuwa wanachama wa BRICS wanapaswa kuzingatia zaidi kuunda miundombinu ya kifedha isiyotegemea taasisi za kimataifa kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia, na pia kutumia sarafu za kitaifa badala ya dola katika mabadilishano yao ya kibiashara.
Kwa hakika, wanachama wa BRICS wanajaribu sio tu kusaidia kuimarisha uhuru wa kifedha wa nchi wanachama, lakini pia kupunguza utegemezi wao kwa mifumo ya kifedha ya Magharibi, hasa dola, kwa kupanua mabadilishano ya kibiashara kati ya wanachama wa BRICS, sera ambayo imemkasirisha sana Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye ametishia kwamba ikiwa nchi za BRICS zitafuata sera ya kufuta dola, atazitoza ushuru wa asilimia 100.
Pamoja na hayo wanachama wa BRICS wanaendelea kuunda mifumo kama vile ya Benki ya Maendeleo ya BRICS, matumizi ya sarafu za kitaifa katika biashara ya pande mbili, kuzindua mifumo huru ya kifedha pamoja na kuanzisha makubaliano ya kutumika fedha za kigeni kati ya nchi wanachama.
Ushirikiano katika afya ya kimataifa ni mhimili mwingine wa unaozingatiwa na wanachama wa BRICS. Mojawapo ya masuala muhimu zaidi baada ya janga la Covid-19 ni kuzingatia afya ya dunia. Kwa kuwa nchi nyingi wanachama wa BRICS zina uzoefu wa kawaida katika uwanja wa kukabiliana na migogoro ya afya, zinajaribu kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na migogoro ya afya kwa kubadilishana ujuzi na rasilimali katika uwanja huu. Kwa hivyo, kuimarishwa ushirikiano wa afya na matibabu ni mhimili mwingine unaozingatiwa na wanachama wa kundi hili.
Kuwa na taathira katika muundo wa amani na usalama wa dunia kwa mtazamo wa pande kadhaa pia ni mhimili mwingine muhimu katika ushirikiano wa wanachama wa kundi la BRICS katika duru hii mpya.
Mwenyekiti mpya wa BRICS pia amesisitiza ushirikiano wa pande kadhaa katika kuimarisha nafasi ya nchi zinazoendelea katika uchukuaji maamuzi ya kimataifa, haja ya kupitiwa upya mfumo wa usalama wa kimataifa na kuunda mifumo ya kiadilifu na yenye taathira zaidi katika kudhibiti migogoro ya kimataifa.
Nchi wanachama wa BRICS pia zitashirikiana katika nyanja za Akili Mnemba AI na mabadiliko ya hali ya hewa. Utawala wa Akili Mnemba (AI) ni mojawapo ya masuala yanayoibuka katika nyanja za kimataifa, ambayo yanahusishwa na changamoto nyingi za kimaadili, kiuchumi na kiusalama. Katika muktadha huu, nchi wanachama wa BRICS zinatakiwa kuunda kanuni na mifumo ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya kuwajibika na matumizi sahihi ya Akili Mnemba. Kuhusu suala hili, kuzingatia masuala ya utawala, kuhakikisha uwazi katika michakato ya maamuzi ya moja kwa moja na kukabiliana na matumizi mabaya ya Akili Mnemba katika nyanja za kijeshi na kijasusi ni mambo yanayopewa umuhimu mkubwa.
Maendeleo ya muundo wa ndani wa kundi la BRICS ili kuimarisha mshikamano kati ya nchi wanachama na kuunda mifumo ya uendeshaji ili kufikia malengo ya pamoja, na vile vile kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa na kutunga sheria sahihi katika uwanja huu pia yamezingatiwa na nchi wanachama wa BRICS.
Inatazamiwa kuwa katika miezi ijayo na kwa kuzingatia matukio ya kisiasa na kiuchumi duniani pamoja na mabadiliko ya mfumo wa kimataifa, na hasa baada ya Donald Trump kushika madaraka kama rais mpya wa Marekani, nchi wanachama wa BRICS zitashirikiana zaidi kimfumo ili kukabiliana na changamoto na migogoro iliyopo.