Kukataa Iraq kushiriki Marekani katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12298-kukataa_iraq_kushiriki_marekani_katika_operesheni_ya_kuukomboa_mji_wa_mosul
Waziri wa Ulinzi wa Iraq Khalid al-Ubaidi amesema nchi hiyo haihitaji ushiriki wa kijeshi wa Marekani kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2016 00:00 UTC
  • Kukataa Iraq kushiriki Marekani katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul

Waziri wa Ulinzi wa Iraq Khalid al-Ubaidi amesema nchi hiyo haihitaji ushiriki wa kijeshi wa Marekani kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul.

Waziri wa Ulinzi wa Iraq ametangaza msimamo huo kufuatia matamshi ya baadhi ya maafisa wa Marekani kuhusu kushiriki vikosi vya jeshi la nchi hiyo katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul.

Kamanda wa Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani, Joseph Votel alitangaza hapo kabla kuwa nchi hiyo na washirika wake wanajiweka tayari kwa ajili ya kushiriki katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul.

Kamanda wa Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani, Joseph Votel

Kukataa waziwazi Waziri wa Ulinzi wa Iraq kushiriki vikosi vya kigeni na hasa vya Marekani katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul kunatokana na tajiriba athirifu iliyopatikana katika operesheni ya kuukomboa mji wa Falujah kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Mji huo wa kistratijia ulioko magharibi mwa Iraq uliweza kukombolewa na kuyatimua kikamilifu magaidi ya kundi la kitakfiri la Daesh katika muda wa takriban mwezi mmoja kwa ushirikiano wa jeshi, vikosi vya wananchi vya al-Hashd al-Shaabi, vikosi vya makabila na vikosi vya kupambana na ugaidi vya Iraq.

Tajiriba ya mapambano ya Falujah imewapa funzo Wairaqi kwamba umoja wa kisiasa na kuwa na nguvu ya pamoja ya kijeshi ndio njia bora kabisa ya kulitokomeza kundi la Daesh katika ardhi ya Iraq; na wala hakuna haja yoyote ya kutegemea ahadi za kujitafutia maslahi na za kisiasa za madola ajinabi likiwemo la Marekani. Uwezo na nguvu ya ndani ni egemeo imara na la kuaminika kwa wananchi kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi yao.

Umoja na mshikamano wa kisiasa ndilo sharti la kufanikiwa Iraq katika nyuga za kisiasa na kijeshi.

Ukweli wa jambo hili umethibitika katika mapambano ya Falujah na kuzidisha maradufu nguvu za vikosi vya kijeshi vya Iraq. Mtazamo huo wa kutegemea nguvu ya ndani na yenye ufanisi uliwezesha kuisambaratisha ngome muhimu ya Daesh magharibi mwa Iraq na kuirejesha Falujah mikononi mwa Wairaq. Leo amani na utulivu umerudi magharibi mwa Iraq, na wakaazi wa mji huo waliolazimika kuwa wakimbizi wanaendelea kurudi majumbani kwao.

Wakaazi wa Falujah wakirudi makwao baada ya mji huo kukombolewa

Kukaririwa tajiriba ya mapigano ya Falujah kutawezesha kufanikiwa pia operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul. Tarehe 10 Juni mwaka 2014, makao makuu hayo ya mkoa wa Nainawa yaliangukia mikononi mwa kundi la kitakfiri la Daesh kufuatia njama ya pamoja ya kundi hilo na maba'athi, na hivi sasa wakaazi wa mji wa Mosul wanatamani ifike haraka siku ya kukombolewa mji wao kutoka mikononi magaidi wauaji wa kundi la kitakfiri la Daesh.

Kanuni zilizowekwa na kundi hilo la kigaidi katika mji wa Mosul zimeyafanya maisha ya wakaazi wa mji huo yawe ya dhiki na tabu; na takwa pekee la wananchi hao kwa serikali na vikosi vya jeshi na usalama vya Iraq ni kuharakishwa operesheni ya mwisho ya kuikomboa Mosul na kutokomezwa kundi la Daesh.

Kwa kuzingatia kuwa vikosi vya jeshi la kujitolea la wananchi vijulikanavyo kama Al-Hashd Al-Shaabi vilipigana bega kwa bega na jeshi na vikosi vya makabila ya mkoa wa al-Anbar katika mapambano ya Falujah dhidi ya Daesh, bila ya shaka kushiriki vikosi hivyo kutarahisisha pia operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul.

Wapiganaji wa vikosi vya kujitolea vya Al-Hashd Al-Shaabi

Ukweli ni kwamba amri iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi imeziba mianya yote ya visingizio na tuhuma zinazotolewa na maadui wa Iraq huru na iliyoungana pamoja dhidi ya Al-Hashd Al-Shaabi. Kwa mujibu wa amri hiyo vikosi hivyo vya kujitolea vya wananchi sasa vitakuwa vikosi rasmi vilivyo chini ya Waziri Mkuu, vikiwa na kamanda, naibu kamanda, brigedi na idara ya uendeshaji. Kutokana na amri iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Iraq vikosi hivyo vya kujitolea vya wananchi vitafanana na vikosi vya nchi hiyo vya kupambana na ugaidi na kwa msingi huo vitapatiwa silaha na mafunzo.

Kuimarishwa nafasi ya vikosi vya Al-Hashd Al-Shaabi kunatokana na ufanisi na uwezo wa vikosi hivyo katika kulinda mipaka ya Iraq; na kuwa na imani na vikosi hivyo kutadhamini kulindwa ardhi yote ya nchi hiyo. Kwa kuzingatia uwezo na nguvu za pamoja za vikosi vyote vya Iraq, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo ametangaza kuwa mwisho wa mwaka huu wa 2016 utakuwa pia ndio mwisho wa maisha ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika ardhi ya Iraq.../