Kimenuka Marekani; Mawaziri wa zamani wa ulinzi wamjia juu Trump
Mawaziri watano wa zamani wa ulinzi wa Marekani wamelaani hatua ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump ya kumfukuza kazi Mkuu wa Majeshi na maafisa wengine wakuu wa jeshi la Marekani.
Mawaziri hao watano wa zamani wa ulinzi wa Marekani wamelaani kitendo cha Donald Trump cha kumfukuza kazi "bila kufikiria" Mkuu wa Majeshi na maafisa wengine wakuu wa jeshi la nchi hiyo na kuliomba Bunge la Congress kuzuia uthibitisho wowote wa warithi wa maafisa hao.
Katika barua yao kali kwa Congress, mawaziri hao wa zamani wa ulinzi pia wamemtuhumu Donald Trump kuwa anataka kulifanya jeshi la Marekani kuwa chombo cha siasa zake za kichama na kutumia njia ya kuwafukuza kazi maafisa "kuondoa mipaka ya kisheria inayobana mamlaka ya rais."
Katika barua hiyo, mawaziri hao wa zamani wameliomba Bunge la Congress kumuwajibisha Trump kwa kuwafurusha "kizembe" maafisa wa jeshi, na wamelisihi lisiidhinishe uteuzi mpya wa viongozi wa Pentagon ila baada ya kupewa maelezo ya kuridhisha.
Barua hiyo imesainiwa na mawaziri watano wa zamani wa ulinzi wa Marekani, William Perry, Leon Panetta, Chuck Hagel, Jim Mattis, na Lloyd Austin.