Mgongano wa maneno na vitendo vya seriakli ya Trump kuhusu Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i123954-mgongano_wa_maneno_na_vitendo_vya_seriakli_ya_trump_kuhusu_iran
Licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kuzungumzia mara kwa mara nia yake ya kufanya mazungumzo na Iran katika miezi ya kwanza ya muhula wake wa pili wa urais na hata kutuma barua kuhusiana na suala hilo kwa Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini kivitendo amekuwa akitekeleza mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran na kuchukua hatua mpya katika uwanja huo kila siku.
(last modified 2025-03-16T02:18:19+00:00 )
Mar 16, 2025 02:18 UTC
  • Mgongano wa maneno na vitendo vya seriakli ya Trump kuhusu Iran

Licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kuzungumzia mara kwa mara nia yake ya kufanya mazungumzo na Iran katika miezi ya kwanza ya muhula wake wa pili wa urais na hata kutuma barua kuhusiana na suala hilo kwa Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini kivitendo amekuwa akitekeleza mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran na kuchukua hatua mpya katika uwanja huo kila siku.

Katika hatua ya hivi karibuni kabisa, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza Jumatano, Machi 12, kuwekewa vikwazo vipya Mohsen Paknejad, Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, makampuni na meli kadhaa zinazohusiana na mauzo ya mafuta ya Iran. Katika taarifa iliyochapishwa na Ofisi ya Wizara ya Kudhibiti Mali za Kigeni (OFAC), inadaiwa kuwa vikwazo hivyo vimewekwa kwa lengo la kuongeza mashinikizo dhidi ya meli ambazo Iran huzitumia kupeleka mafuta China. Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa "mashinikizo ya juu" ya serikali ya Marekani, ambayo inataka eti kupunguza mauzo ya mafuta ya Iran hadi kufikia sifuri. Kwa mujibu wa taarifa hii, Mohsen Paknejad, ambaye anasimamia wizara ya mafuta ya Iran tangu majira ya joto mwaka huu, amekuwa na nafasi muhimu katika kutenga mabilioni ya dola za mafuta kwa ajili ya vikosi vya jeshi la Iran, ikiwa ni pamoja na Walinzi wa Mapinduzi IRGC.

Kadhalika, ikiwa ni katika fremu ya kubana mauzo ya mafuta ya Iran, makampuni na meli kadhaa zimekuwa zikilengwa katika maeneo tofauti ya dunia, zikiwemo China, Hong Kong, India, Bangladesh, Seychelles na Suriname. Serikali ya Marekani imeonya kwamba ukiukaji wowote wa vikwazo hivi unaweza kusababisha kutozwa faini ya kiraia au ya jinai dhidi ya watu binafsi na vyombo vinavyohusika katika miamala hii.

Trump, katika muhula wake wa pili wa madaraka, ametoa madai ya kutaka kutatua matatizo yaliyopo kati ya Marekani na Iran kupitia mazungumzo, lakini katika kauli zake zote na hata katika barua yake ya karibuni kwa Iran, ametumia lugha ya kuamrisha na kutaka matakwa ya Marekani yazingatiwe bila kujali matakwa ya Iran.

Katika mahojiano na Fox Business, Trump alisema Jumatano kwamba alikuwa  amemwandikia barua Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akitaka mazungumzo ya pande mbili yafanyike. Alisema katika mahojiano hayo kwamba: "Ninapendelea kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano na Iran. Chaguo jingine ni kwamba ufanye kitu. Kwa sababu haiwezekani Iran kuwa na silaha za nyuklia." Inaonekana kuwa hatua ya Trump kutangaza kumwandikia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imechukuliwa kwa lengo la kutaka kuonyesha kuwa Washington inafadhilisha diplomasia na hivyo kutupa mpira wa mazungumzo katika uwanja wa Iran. Kwa hakika, kwa kuitishia Tehran, Trump anajaribu kuitwisha masharti yake.  Barua ya Trump hatimaye iliwasilishwa kwa Iran kupitia mjumbe wa serikali ya UAE.

Makabiliano ya Iran na Marekani

Siku moja baada ya kutangazwa habari ya Trump kutuma barua, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: "Ukweli kuwa baadhi ya serikali zenye kiburi zinasisitiza kufanya mazungumzo, mazungumzo yao si ya kutatua matatizo, bali ni ya kudhibiti wengine. Mazungumzo yafanyike ili wafikie kile wanachokitaka."  Amesisitiza kwa kusema: "Mazungumzo yanayofuatiliwa na Marekani hayataishia kwenye mpango wa nyuklia wa Iran. Serikali hizi hazina nia ya kufanya mazungumzo ya kutatua matatizo bali zinataka kutawala na kulazimisha."

Siku ya Jumatano, Machi 12, Ismail Beqaei, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran alitangaza kuwa barua ya Donald Trump ilitumwa Tehran kupitia Anwar Gargash, mshauri wa kidiplomasia wa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ayatullah Khamenei kwa mara nyingine tena amepinga mazungumzo na Marekani, akiashiria kutokuwepo imani na uhakika wa kuondolewa vikwazo vya nchi hiyo ya Magharibi dhidi ya Iran. Kuhusiana na suala hilo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika moja ya hotuba zake za hadhara: “Baadhi ya watu ndani ya nchi wanaendelea kung'ang'ania suala la kufanya mazungumzo na kusema, kwa nini hamjibu? Kwa nini msizungumze? Kwa nini msiketi kwenye meza ya mazungumzo na Marekani? Ikiwa lengo la mazungumzo ni kuondoa vikwazo, mazungumzo na serikali hii ya Marekani hayataondoa vikwazo, yaani hayataondoa vikwazo. Vikwazo vitaongeza, mashinikizo yataongezeka, mazungumzo na serikali hii yataongeza mashinikizo."

Kwa maelezo hayo na kwa mujibu wa mtazamo wa Iran, mazungumzo yanayofuatiliwa na Trump ni mbinu tu ya Marekani kulazimisha matakwa yake kwa Tehran na hata kuongeza mashinikizo na kukaza fundo la vikwazo. Aidha, tangazo la vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran hata wakati Trump anapotoa madai ya kufanya mazungumzo na Iran linaonyesha kuwa Washington inalenga tu kuzidisha mashinikizo na kutaka kuitwisha Iran matakwa yake.